Ahadi ya India ya kuondoa marufuku ya mawasiliano eneo la Kashmir
Baada ya kupita zaidi ya miezi miwili ya kutekelezwa marufuku ya mawasiliano katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India, hatimaye serikali ya New Delhi imetangaza kufuta baadhi ya vizuizi vilivyowekwa katika uwanja huo.
Rohit Kansal, msemaji wa serikali ya Jammu na Kashmir ameviambia vyombo vya habari kwamba, mawasiliano yote ya simu za mkononi yatafunguliwa leo Jumatatu Oktoba 14 katika baadhi ya maeneo ya Kashmir. Hata hivyo afisa huyo wa serikali ya India ameongeza kuwa, mawasiliano ya simu za mkononi yatadhibitiwa na serikali ya India katika maeneo 10 ya eneo hilo. Tarehe 5 Agosti mwaka huu, serikali ya India ilifuta hadhi ya mamlaka ya ndani na madaraka maalumu ya eneo la Jammu na Kashmir. Kufuatia hatua hiyo ambayo iliibua malalamiko ya wakazi wa Kashmir yote, serikali ya India sambamba na kupitisha sheria ya kutotoka nje usiku, iliwatia mbaroni pia makumi ya watu wa eneo hilo. Aidha serikali ya India ilikata mawasiliano yote, yakiwemo mawasiliano ya simu za mkononi katika eneo la Kashmir lililo chini ya udhibiti wake. Ahadi ya serikali ya India ya kurudisha tena mawasiliano katika eneo la Jammu na Kashmir, imetolewa siku chache baada ya mahakama kuu ya nchi hiyo kumtaka Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India kufutilia mbali sheria ya kutotombea usiku katika eneo hilo sambamba na kurejesha hali ya kawaida katika eneo hilo.
Mahakama kuu hiyo iliitaja hatua ya serikali ya New Delhi ya kutangaza hali ya hatari na kisha kukata mawasiliano yote ya Kashmir baada ya kuliondolea eneo hilo utawala wa ndani, kuwa iliyo kinyume cha sheria na ambayo imevuruga maisha ya kawaida ya wakazi wa eneo hilo kutokana na vikwazo vingi wanavyokabiliwa navyo. Aidha malalamiko ya ndani nchini India ya kupinga hatua ya uchochezi ya chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) ya kufuta sheria ya kujitawala eneo la Kashmir na kisha kutekeleza utawala wa kijeshi sambamba na kukata mawasiliano katika eneo hilo, hayakukomea tu kwenye mahkama kuu ya nchi hiyo, bali makundi mengi, asasi za kutetea haki za binaadamu na vyama vilivyo na wabunge kwenye kongresi, vinapinga vikali suala hilo vikisema kuwa lina taathira hasi na kuhatarisha maslahi ya kitaifa ya India. Uamuzi wa kuondoa baadhi ya marufuku ya mawasiliano katika eneo la Jammu na Kashmir unatokana na kwamba serikali ya India haikuweza kupinga hukumu ya mahakama kuu iliyoitaka kufutilia mbali sheria ya hali ya hatari katika eneo la Kashmir.
Hata kama serikali ya India haijaondoa marufuku yote iliyotokana na kutekelezwa hali ya hatari katika eneo la Kashmir, lakini kulazimika chama tawala cha BJP kutekeleza hukumu ya mahakama kuu, kunaonyesha uwepo wa mashinikizo makubwa ya kisiasa, kijamii na kimahakama ndani na nje ya serikali ya Narendra Modi. Katika hali ambayo serikali ya India imekuwa ikitoa mashinikizo ya kila upande dhidi ya wakazi wanaodhulumiwa wa Kashmir ili kuwalazimisha wakubaliane na hali mpya iliyojitokeza, lakini baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisiasa na kiusalama wanasema kuwa ukandamizaji huo si tu kwamba hautasaidia kupunguza malalamiko ya wakazi wa eneo hilo, bali utaimarisha tu azma yao ya kuendelea kupigania haki yao ya kimsingi kwa ajili ya kuainisha mustakbali wao. Serikali ya Pakistan pia inafanya juhudi za kimataifa na kupitia mashinikizo ya walimwengu juu ya faili la Kashmir ili iweze kuilazimisha serikali ya India iangalie upya uamuzi wake wa kulifutia haki ya kujitawala eneo la Kashmir. Pendekezo la zaidi ya wajumbe 50 wa Kamati ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufutwa haraka kifungo cha nyumbani dhidi ya wakazi wa eneo hilo, ni miongoni mwa mafanikio ya juhudi hizo za Islamabad.