Trump aendelea kutoa misimamo ya nyuso mbili kuhusu Wakurdi wa Syria
Rais wa Marekani kwa mara nyingine tena ametia ulimi puani na kubadilisha msimamo wake wa huko nyuma kuhusu Wakurdi wa Syria. Katika ujumbe wake mpya wa Twitter sasa Trump amewataka Wakurdi hao waende wakajikusanye kwenye maeneo yenye utajiri wa mafuta.
Katika ujumbe wake wa jana wa Twitter, Donald Trump alisema, maeneo yenye utajiri wa mafuta ya kaskazini mwa Syria yalikuwa mikononi mwa Daesh (ISIS) kabla Marekani haijawasaidia Wakurdi kuyateka maeneo hayo. Kabla ya hapo Trump alikuwa amesema, wako kaskazini mwa Syria kwa ajili ya mafuta na si kwa ajili ya kuwalinda Wakurdi.
Vile vile alikuwa amesema kwamba ni idadi ndogo tu ya wanajeshi wa Marekani watakaobakia katika maeneo yenye utajiri wa mafuta ya kaskazini mwa Syria.
Hata hivyo katika ujumbe wake mpya wa Twitter amebadilisha msimamo na kusema kuwa, wanajeshi wa Marekani wataendelea kuweko kwenye maeneo hayo na hawatoruhusu magaidi wa Daesh wayateke tena.
Misimamo hiyo ya Trump inayokinzana kila kukicha inatokana na lawama alizopata kutoka kwa wanasiasa wa Marekani ambao katika kipindi cha siku za hivi karibuni wamekuwa wakimlaumu sana kwa kuwapiga teke na kuwatelekeza waasi hao wa Kikurdi licha ya kwamba ni vibaraka wakubwa wa Marekani.
Awali Trump alikuwa ameafikiana na mashambulizi ya Uturuki dhidi ya waasi hao, lakini baada ya kulaumiwa vikali ndani na nje ya Marekani alibadilisha msimamo wake na kuilazimisha Uturuki isitishe mashambulizi hayo.
Kila leo rais huyo wa Marekani anazuka na matamshi na misimamo mipya kuhusu maeneo ya kaskazini mwa Syria.