Trump adai pia habari ya kuuawa mrithi wa Abubakar al-Baghdadi
Rais Donald Trump wa Marekani ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba askari wa Kimarekani wamemuua pia mrithi wa Abubakar al-Baghdadi, kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).
Rais huyo wa Marekani ameeleza kwamba, kuna uwezekano mkubwa mrithi wa al-Baghdadi na ambaye alikuwa na nafasi kubwa ndani ya kundi hilo akawa ameuawa. Hii ni katika hali ambayo, Trump bado hajalitaja jina la mrithi huyo wa Abubakar al-Baghdadi anayedai kuuawa. Kabla ya hapo pia, afisa wa ngazi ya juu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na ambaye hakutaja jina lake alinukuliwa akisema kuwa, Abul-Hasan al-Muhajir, msemaji wa kundi la Daesh (ISIS) aliangamizwa katika mji wa Jarabulus mkoani Aleppo, kaskazini mwa Syria. Jumapili iliyopita pia afisa mmoja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) alidai kwamba, kiongozi wa kundi la Daesh (al-Baghdadi) aliuawa na jeshi la Marekani kaskazini magharibi mwa mkoa wa Idlib nchini Syria.
Saa moja baadaye Rais Donald Trump wa nchi hiyo alithibitisha habari ya kuuawa kinara wa kundi hilo katika operesheni iliyofanywa na askari wa Kimarekani. Hata hivyo Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitoa taarifa iliyotilia shaka mafanikio ya operesheni hiyo ya askari wa Marekani nchini Syria. Kundi la kigaidi la Daesh miaka ya hivi karibuni lilivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya nchi za Iraq na Syria likisaidiwa na Marekani, Saudi Arabia, utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wao na kufanya jinai za kutisha katika nchi hizo na kwingineko duniani.