Kuanza duru mpya ya maandamano ya upinzani nchini Ufaransa
Uamuzi mpya wa serikali ya Ufaransa wa kuifanyia marekebisho sheria ya kustaafu, umeibua wimbi jipya la maandamano na migomo nchini humo ambavyo vilianza tangu siku ya Alkhamisi iliyopita.
Katika maandamano hayo ambayo bado yanaendelea, maelfu ya raia wa Ufaransa wamemiminika barabarani kutangaza upinzani wao kwa muswada huo pamoja na utendajikazi wa serikali ya Rais Emmanuel Macron kwenye uga wa kiuchumi. Kwa mujibu wa mpango wa kurekebisha mfumo wa ustaafu, serikali ya Ufaransa inakusudia katika marekebisho hayo kufidia nakisi ya bajeti kwa kupunguza gharama za matumizi yake; na mbali na kuongeza miaka ya utumishi na kupunguza mishahara ya wastaafu, inapanga pia kupunguza wafanyakazi wa sekta za elimu na mafunzo na afya ya jamii. Wimbi jipya la maandamano ya wananchi ndani ya Ufaransa limeibuka katika hali ambayo nchi hiyo imekuwa uwanja wa maandamano makubwa tangu tarehe 17 Novemba mwaka jana, maandamano ya wananchi yaliyopewa jina la Harakati ya Vizibao vya Njano. Harakati hiyo ambayo iliibuka kufuatia kuongezwa kodi ya nishati ya mafuta kwa senti 6, imekuwa ikifanya maandamano kila Jumamosi kwa zaidi ya mwaka sasa katika miji tofauti ya Ufaransa. Hata kama harakati na malalamiko hayo ya nchi nzima ndani ya Ufaransa hatimaye yalimlazimisha Rais Emmanuel Macron aachane na uamuzi wake huo, lakini waandamanaji hawajaridhishwa na siasa za serikali ya rais huyo kijana.
Hivi sasa muswada wa marekebisho ya sheria ya ustaafu umeibua harakati nyingine ya vizibao katika anga ya kisiasa na kijamii nchini Ufaransa. Ukiondoa chama cha Republican chenye mafungamano na Rais Macron, akthari ya vyama vya siasa vimepinga marekebisho hayo, huku kwa upande wake serikali ikitangaza kwamba muswada huo utafikishwa bungeni mwezi Januari mwakani. Waandamanaji wanasema kuwa marekebisho ya sheria ya ustaafu, yataongeza umasikini kwa wananchi. Aidha watu wengi wanaamini kuwa mabadiliko ya sheria hiyo yatakuwa na madhara kwa wananchi wengi na yatalinufaisha kundi dogo tu la watu. Kuhusiana na suala hilo, Philippe Martinez Katibu wa Jumuiya ya Wafanyakazi amesema: "Serikali inapaswa ifute muswada wa marekebisho ya sheria ya kustaafu ambayo inaufanya mfumo wa pensheni kuwa wa kibinafsi. Muswada huo utaongeza umasikini nchini Ufaransa." Maandamano nchini Ufaransa yamekwamisha shughuli za sekta tofauti kuanzia shule, vyuo vikuu na shughuli za usafirishaji. Waandamanaji wanasema kuwa maandamano hayo hayatokoma hadi pale serikali itakapotangaza kufuta muswada huo. Hii ni katika hali ambayo ikulu ya Élysée imetangaza kuwa Rais Emmanuel Macron ataamiliana kwa utulivu na uthabiti na malalamiko hayo na yuko tayari kufanya mazungumzo juu ya suala hilo. Aidha imeongeza kuwa rais huyo anaheshimu nidhamu ya kijamii na malalamiko ya Wafaransa. Katika uwanja huo siku chache zijazo Édouard Philippe, Waziri Mkuu wa Ufaransa amepanga kuweka wazi mpango kamili wa serikali ya Paris kuhusiana na marekebisho hayo. Weledi wengi wa masuala ya kisiasa wameitaja idadi ya waandamanaji katika maandamano ya siku tatu zilizopita kuwa ni kubwa zaidi tangu mwaka 2003, na kwamba ushiriki mkubwa huo katika barabara za Ufaransa, ni pigo kubwa kwa serikali ya Rais Emmanuel Macron.
Jean-Michel Blanquer, Waziri wa Elimu nchini Ufaransa amesema kuwa: "Hatuwezi kukana kuwa mgomo huu ni mkubwa sana, haujawahi kushuhudiwa tangu mwaka 2003." Katika siku zijazo serikali ya Ufaransa itawalisilisha taarifa kamili kuhusu mpango wa ustaafu, kama ambavyo pia itafanya vikao mbalimbali na viongozi wa jumuiya za wafanyakazi wa nchi hiyo. Bila kujali nini itakuwa natija ya mazungumzo hayo, inavyoonekana, harakati za malalamiko ya kila mara nchini Ufaransa na katika baadhi ya nchi za Ulaya zimezidi kushika kasi. Hata kama marekebisho ya ongezeko la ushuru pamoja na marekebisho ya sheria ya ustaafu ndio sababu ya kuibuka harakati za maandamano ya kupinga siasa za serikali ya Paris, lakini ukweli ni kwmba maandamano nchini Ufaransa yanapinga harakati ya Kibepari, ongezeko la ufa wa kimatabaka na kutokuwepo uadilifu wa kijamii ambavyo vimepelekea kuongezeka umasikini nchini humo. Na hii ni katika hali ambayo kwa muda sasa Rais Emmanuel Macron amekuwa akijaribu kujionyesha kuwa yeye ni mmoja wa viongozi wenye nguvu zaidi barani Ulaya. Inavyoonekana, wakati mgumu zaidi utamkabili rais huyo kijana na jamhuri ya Ufaransa katika siku za usoni.