Kusitishwa vita vya kibiashara kati ya China na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57896-kusitishwa_vita_vya_kibiashara_kati_ya_china_na_marekani
Hatua ya Marekani na China kutangaza kufikiwa makubaliano ya awali ya kibiashara, imesitisha vita vya kibiashara kati ya pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2019 08:24 UTC
  • Kusitishwa vita vya kibiashara kati ya China na Marekani

Hatua ya Marekani na China kutangaza kufikiwa makubaliano ya awali ya kibiashara, imesitisha vita vya kibiashara kati ya pande mbili.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa siku ya Ijumaa kati ya Washington na Beijing, Marekani itatakiwa kupunguza ushuru kwa baadhi ya bidhaa za China zinazoingizwa nchi hiyo, kama ambavyo pia imekubali kufuta utekelezwaji wa ushuru wa forodha uliotakiwa kuanza kutozwa leo Disemba 15. Robert Lighthizer, mwakilishi wa ngazi ya juu wa kibiashara wa Marekani kwenye mazungumzo hayo amenukuliwa akisema kuwa China pia imeahidi kuongeza ununuzi wa bidhaa za Marekani katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Rais Donald Trump wa Marekani amezungumzia makubaliano hayo ya awali ya kibiashara kati ya nchi mbili na kudai kuwa, katika nyuga nyingi Beijing imeahidi kufanya mabadiliko ya kimuundo na ununuzi wa bidhaa za kilimo, nishati na bidhaa nyingine zinazozalishwa nchini Marekani. Aidha Trump amesema kuwa, China itanunua bidhaa za kilimo kutoka Marekani zenye thamani ya dola bilioni 50. Hata kama makubaliano ya China na Marekani ya kuhitimisha vita vya kibiashara baina ya nchi mbili ambavyo vilianza mwaka jana, yanaweza kupunguza kwa kiasi fulani mwenendo wa kushtadi mzozo baina yao, lakini ni wazi kuwa makubaliano hayo yanaweza kuvunjika wakati wowote.

Viongozi wa China na Marekani ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja  wamekuwa wakivutana katika vita vya kibiashara

Kuhusiana na suala hilo Shi Yinhong, Mshauri wa Serikali ya China na Muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Beijing anasema: "Makubaliano hayo ni ya muda na ya kutuliza mambo tu. Mivutano ya muda mrefu ambayo ipo kati ya Washington na Beijing haiwezi kumalizika kwa kutiwa saini makubaliano hayo. Ukweli ni kwamba makubaliano ya awali kati ya China na Marekani yameakhirisha tu tofauti za pande mbili, hitilafu ambazo bila shaka zitadhihiri tena katika siku zijazo na hasa ikitiliwa maanani kuwa matatizo yataibuka tena."  Na hasa tunapotambua kwamba Rais Donald Trump wa Marekani anajulikana kwa kukiuka ahadi na kutofungamana na mikataba iliyotiwa saini na serikali za kabla yake na ya sasa ya nchi hiyo katika nyuga tofauti. Mifano ya wazi kuhusiana na suala hilo ni kujiondoa kwake katika mikataba ya pande kadhaa ya kimataifa ukiwemo mkataba wa tabianchi wa mjini Paris, mkataba wa Trans-Pacific, mapatano ya nyuklia ya JCPOA na mkataba wa North American Free Trade Agreement (NAFTA). Shi Yinhong, mshauri wa serikali ya China na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Beijing ameashiria makubaliano hayo ya awali ya kupanua ushirikiano na Marekani na kusimamishwa kwa muda vita vya kibiashara kati ya pande mbili na kusema: "Trump ni mtu kigeugeu na mwenye fikra ya kukwepa majukumu."

Utiwaji saini makubaliano hayo ya awali huenda ukawaleta pamoja viongozi wa nchi mbili

Licha ya kufikiwa mapatano ya muda katika uwanja huo, lakini bado viongozi wa China wana wasiwasi kuwa huenda Trump akachukua hatua ya upande mmoja na kuyavunja mapatano hayo kutokana na mwenendo ambao unautekelezwa katika siasa za kigeni na kibiashara za White House. Aidha siasa hizo za upande mmoja za Marekani, zimekosolewa vikali na jamii ya kimataifa. Hata hivyo matamshi ya Trump kwamba nchi yake ilikuwa inahitaji mapatano kama hayo, yanaweza kuwa ni ishara ya wazi ya hali ngumu iliyokuwa inaikabili ikulu ya White House kama vita vya kibiashara vingeendelea kati ya nchi mbili na matokeo yake hasi kuathiri sekta tofauti za Marekani. Kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, akthari ya wataalamu wa masuala ya kiuchumi nchini Marekani wamekosoa vikali siasa za rais wa nchi hiyo za kuzipandishia ushuru wa forodha bidhaa za China na kutahadharisha kwamba mwenendo huo unaweza kuusababishia madhara makubwa uchumi wa nchi hiyo. Kwa kuzingatia hali ngumu inayomkabili Trump kuhusiana na uchaguzi wa rais wa 2020, na suala la kusailiwa kwake katika kongresi ya nchi hiyo, hatua yake ya lulegeza msimamo katika vita vya kibiashara alivyovianzisha mwenyewe na China, inatokana na juhudi zake za kujaribu kuboresha nafasi yake ya kisiasa katika uga wa ndani ya Marekani.