Jarida la Christianity Today la Marekani lamponda tena Trump
Jarida la Kiinjilisti la Christianity Today la Marekani kwa mara nyingine tena limemkosoa vikali Rais Donald Trump wa nchi hiyo, likisisitiza kuwa mwanasiasa huyo wa Republican anapaswa kuondolewa ofisini.
Mkuu wa jarida hilo ambalo ndilo kubwa zaidi la Kikristo nchini Marekani, Timothy Dalrymple ameandika makala ambayo imekosoa vikali mienendo hasi ya Trump, likisisitiza kuwa mwanasiasa huyo ni mtu asiye na maadili, fisadi, mroho, mbaguzi na mwenye chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahajiri.
Kadhalika amewakosoa viongozi wa Kikristo wanaojipendekeza kwa Trump na kusisitiza kwamba, "Muamana usio na masharti na mipaka unapaswa tu kuwa kati yao na Mungu."
Mwandishi wa makala hiyo yenye kichwa kisemacho "Bendera Kwenye Upepo Mkali", amebainisha kuwa: Ni jambo moja kupongeza mafanikio yake (Trump) na ni jambo jingine kuruhusu na kupuuza utumiaji wake mbaya wa mamlaka.
Katika tahariri nyingine iliyochapishwa na jarida hilo la Kiinjilisti la Christianity Today la Marekani wiki iliyopita, Mhariri Mkuu, Mark Galli aliandika kuwa, Trump ni mtu asiye na maadili na ambaye anapaswa kuuzuliwa.
Tafiti mbalimbali za maoni zilizofanywa nchini Marekani hivi karibuni zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya Wamarekani wamepoteza imani na uongozi wa Trump na wanataka auzuliwe.