Russia yamkosoa Guterres kwa kufumbia macho ukiukaji sheria unaofanywa na Marekani
Kwa kuzingatia kuwa Marekani ndiko yaliko makao makuu ya Umoja wa Mataifa, nchi hiyo ya kibeberu daima imekuwa ikiwawekea vikwazo wanadiplomasia na maafisa wa ngazi za juu wa nchi zinazopinga siasa za Washington, wanaoazimia kusafiri nchini humo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
Katika miezi ya hivi karibuni serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo imekuwa ikitekeleza siasa za ukandamizaji na kuwabana wanadiplomasia na maafisa wa ngazi za juu wa Russia kwa kadiri kwamba imekuwa akiwazuia kusafiri au kudhibiti safari zao katika maeneo tofauti ya New York, makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Jambo hilo limeipelekea Russia kulalamika na kuukosoa vikali Umoja wa Mataifa.
Kuhusu suala hilo, Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amemkosoa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutokana na kimya chake mbele ya ukiukaji huo wa wazi wa Marekani wa hati ya umoja huo. Akizungumza Jumatano, Maria Zakharova alisema kuwa hatua ya Marekani kutowapa visa, maafisa wa Russia ni ukiukaji wa wazi wa hati ya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa Marekani inachelewesha kwa makusudi utoaji wa viza kwa maafisa hao huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akifumbia macho hatua hiyo ya Marekani isiyo ya kisheria.
Moscow imeonya kwamba huenda hatua hiyo ikaharibu uhusiano usio mzuri sana kati ya pande mbili. Mwezi Septemba mwaka huu Russia ilimwita mwanadiplomasia wa Marekani nchini humo na kumuelezea malalamiko ya Moscow kuhusiana na hatua ya Marekani ya kutowapa viza maafisa kadhaa wa Russia waliokuwa wamepanga kuelekea Marekani kwa ajili ya kushiriki kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Marekani ima hunyima au kuchelewesha kwa makusudi viza za wanadiplomasia wa Russai na wa nchi nyingine zinazopinga siasa za mabavu za nchi hiyo wanaokusudia kusafiri mjini New York kwa ajili ya kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa. Marekani inatekeleza siasa hizo za uvunjaji sheria za kimataifa katika hali ambayo nchi hiyo kwa mujibu wa sheria za uenyeji za Umoja wa Mataifa, inalazimika kutoa visa na kuruhusu wageni walioalikwa na umoja huo wahudhurie vikao vyake bila kuwasumbua na kuwabana kwa njia yoyote ile. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinalipa jambo hilo umuhimu mkubwa.
Tarehe 18 Disemba mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kulaani hatua ya Marekani ya kuwanyima viza wanasiplomasia wa Russia na pia kuitaka ifutilie mbali siasa zake za kuwazuia wanadiplomasia wa Iran kuingia nchini humo. Aziomio hilo ambalo liliwasilishwa kwenye baraza hilo na wawakilishi wa Cyprus, Bulgeria, Canada, Ivory Coast na Costa Rica lilipasishwa kwa sauti moja na bila ya kupigiwa kura. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa Umoja wa Mataifa unaitaka Marekani kuondoa vikwazo vyote vilivyowekewa jumbe na maafisa wa baadhi ya nchi.
Kupitishwa azimio hilo tena kwa sauti moja kunathibitisha wazi kwamba siasa za mabavu za Marekani za kutaka kuwawekea vikwazo maafisa na wanadiplomasia wa baadhi ya nchi zinazopinga siasa au washindani wa Marekani wanaotaka kusafiri mjini New York kwa lengo la kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa zinapingwa vikali kimataifa.
Inaonekana kuwa lengo hasa la siasa hizo za Marekani ni kujaribu kuzuia kuwepo ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya maafisa na wanadiplomasia wa ngazi za juu wa nchi hizo pinzani za Marekani na wenzao kutoka pembe nyingine za dunia. Ikiwa ni katika kutekeleza siasa zake hizo, katika hatua ya kwanza viongozi wa Marekani huchukua hatua ya kuwanyima viza maafisa na wanadiplomasia wa nchi pinzani, na inapokabiliwa na mashinikizo kutoka kwa nchi zilizo na nguvu ya kisiasa kama Russia na Iran bazi hulazimika kulegeza msimamo na kuchukua hatua ya pili ambayo ni kutoa viza za wanadiplomasia hao kwa kuchelewa au kupunguza idadi yao ili eti kupunguza athari ya kuwepo kwao mjini New York.
Suala muhimu hapa ni uzembe wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na ukiukaji huo wa wazi wa Marekani wa sheria za umoja huo. Kama alivyosema Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ta Russia, kidole cha lawama na ukosoaji kinapaswa kuelekezewa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye haichukulii Marekani hatua yoyote ya kisheria na kwa hakika anafumbia macho ukiukaji huo wa wazi wa Washington wa sheria za umoja huo.