Baridi na maporomoko ya theluji yaua watu 67 nchini Pakistan
Kwa akali watu 67 wamepoteza maisha kutokana na baridi kali ya msimu wa kipupwe pamoja na maporoko ya theluji katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan ndani ya masaa 24 yaliyopita.
Maafisa wa serikali ya Pakistan wamesema watu kadhaa wametoweka kutokana na maporomoko hayo, huku wengine wakikwama katika vijiji vilivyoko katika Bonde la Neelum, kaskazini mwa eneo la Kashmiri la upande wa Pakistan kutokana na janga hilo la kimaumbile.
Huku hayo yakiarifiwa, watu kumi wakiwemo wanajeshi watano wamefariki dunia kutokana na maporomoko mengine ya theluji katika eneo la Jammu na Kashmir inayodhibitiwa na India.
Mwaka 2012, maporomoko makubwa ya theluji yaliyakumba makao makuu ya vikosi vya jeshi la Pakistan mpakani na India, ambapo wanajeshi 124 na raia 11 waliaga dunia.
Wakati huo huo, Wizara ya Kudhibiti Majanga ya Afghanistan imesema watu 15 wamepoteza maisha kutokana na maporomoko ya theluji usiku wa kuamkia leo, na kupelekea idadi ya walioaga dunia kutokana na janga hilo nchini humo tokea Jumapili iliyopita kufikia watu 39.
Zaidi ya nyumba 300 zimeharibiwa kutokana na mafuriko, maporomoko ya theluji na maporomoko ya udongo katika maeneo mbali mbali ya Afghanistan.