Maelfu ya wanawake waandamana dhidi ya Trump nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58610-maelfu_ya_wanawake_waandamana_dhidi_ya_trump_nchini_marekani
Makumi ya maelfu ya wanawake wameshiriki maandamano katika miji mikubwa ya Marekani ukiwemo mji mkuu Washington, kupinga sera za kibaguzi za Rais Donald Trump wa nchi hiyo dhidi ya wanawake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2020 04:32 UTC
  • Maelfu ya wanawake waandamana dhidi ya Trump nchini Marekani

Makumi ya maelfu ya wanawake wameshiriki maandamano katika miji mikubwa ya Marekani ukiwemo mji mkuu Washington, kupinga sera za kibaguzi za Rais Donald Trump wa nchi hiyo dhidi ya wanawake.

Mjini Washington wanawake hao sambamba na kupinga sera hizo za kibaguzi za Trump, wamekosoa pia namna utawala wa mwanasiasa huyo wa Republican usivyotilia maanani suala muhimu la mabadiliko ya tabianchi.

Moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao lilikuwa na maandishi yanayosema: Sote tulifahamu kuwa Trump atakuwa mtawala mbaya, lakini hatukutazamiwa ingefikia kiwango hiki.

Maandamano haya dhidi ya Trump hufanyika kila mwaka, ambapo washiriki huonesha kutoridhishwa kwao na sera za kibaguzi za Trump na hususan misimamo yake ya chuki na udhalilishaji dhidi ya wanawake, wahajiri na Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Waandamanaji waliobeba mabango yanayomkashifu Trump

Waandamanaji hao wanasema Trump ametumia mamlaka yake kuchochea hofu, ubaguzi wa kijinsia na chuki dhidi ya wageni na wahamiaji kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.

Maandamano haya ya wanawake dhidi ya Trump yalifayika mara ya kwanza Januari 21 mwaka 2016, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuanza kazi Trump katika Ikulu ya White House. Zaidi ya wanawake 66 elfu walishiriki maandamano hayo.