Uongo wa Trump alioutamka katika hotuba ya kila mwaka waanikwa
Mtandao mmoja wa habari wa Marekani umeweka wazi idadi ya uongo uliosemwa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo katika hotuba yake ya kila mwaka.
Mtandao wa habari wa Now This umeweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter video na kufafanua kuwa katika kila dakika mbili na nusu za hotuba yake ya kila mwaka Trump alisema uongo mara moja. Trump ambaye amepata umashuhuri kwa kusema uongo kila mara katika madai yake, hivi karibuni pia alitoa madai ambayo hayana ukweli wowote katika hotuba yake ya kila mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa uongo uliosemwa na rais huyo wa Marekani ni kuhusiana na uzalishaji mafuta, ongezeko la ajira na masuala yanayohusu uchumi wa Marekani. Tarehe nne ya mwezi huu Trump alitoa hutuba yake ya tatu ya kila mwaka ndani ya bunge la Kongresi la Marekani kwa lengo la kuelezea hali jumla ya nchi hiyo. Hotuba hiyo ya Trump iliyojaa majivuno na kujisifu kuhusiana na utendajikazi wake, ilikosolewa vikali na viongozi wa chama cha Democrat.