Guterres ataka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuna haja ya kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, vikwazo hivyo vimekuwa kizingiti katika jitihada za Jamhuri ya Kiislamu za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi cha Corona.
Antonio Guterres amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambapo wamezungumzia changamoto inazokabiliana nazo Iran kutokana na vikwazo wakati huu wa mapambano dhidi ya maabukizi ya kirusi cha Corona.
Guterres ameashiria kuwa yuko pamoja na taifa la Iran katika kipindi hiki kigumu cha kukabiliana na mlipuko wa Corona na kueleza bayana kuwa, kuna udharura wa kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran.
Kwa upande wake, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kuzishuruku taasisi zinazofungamana na Umoja wa Mataifa kwa misaada yao kwa Iran, lakini pia amesisitizia udharura wa kukomesha ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Iran, ili taifa hili liweze kukabiliana na maradhi ya Corona.
Katika ujumbe wake wa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema dunia inakabiliana na mgogoro mkubwa wa afya ambao haujawahi kushuhudiwa katika kipindi chote cha historia.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, watu wasiopungua 255,000 wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 kote duniani na miongoni mwao zaidi ya 10,000 wameaga dunia.