OIC yalaani ukatili unaozidi kufanywa dhidi ya Waislamu nchini India
Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani ukatili unaozidi kufanywa dhidi ya Waislamu wa India sambamba na kuenea maambukizo ya virusi vya corona vya COVID-19 nchini humo.
Kamisheni Huru ya Kudumu ya Haki za Binadamu ya OIC imetoa taarifa ikieleza kwamba, ni jambo la kuaibisha kueneza chuki dhidi ya Uislamu nchini India na kuwatuhumu Waislamu kuwa ndio walioeneza virusi vya corona katika nchi hiyo. Taarifa hiyo imeitaka serikali ya New Delhi ichukue hatua kuidhaminia haki zake jamii ya Waislamu wa India.
Kamisheni ya haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesisitiza katika taarifa yake hiyo iliyotumwa kupitia akaunti yake ya Twitter kwamba, mielekeo hasi ya vyombo vya habari vya India nayo pia inawafanya Waislamu waandamwe na vitendo vya ukatili na ubaguzi.

Katika siku za karibuni, wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka wamekuwa wakilitumia vibaya janga la corona kwa kuwatuhumu Waislamu kuwa wamekula njama dhidi ya nchi hiyo na kwa kisingizio hicho kuwashambulia na kuwaandama Waislamu hao kwa kuwafanyia hujuma mbalimbali.
Mnamo mwezi Februari, mji mkuu wa India New Delhi ulishuhudia hujuma na mashambulio ya kikatili ya wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka dhidi ya Waislamu, yaliyosababisha vifo vya Waislamu 54.
Chanzo hasa cha machafuko hayo yaliyozuka katika mwezi huo wa Februari kilikuwa ni kupitishwa sheria mpya ya uraia ambayo inawapa kipaumbele cha kupata uraia wa India raia wa kigeni wasio Waislamu. Waislamu wa India wanaitakidi kuwa lengo la hatua hiyo ya serikali ya New Delhi ni kuitenga na kuikandamiza jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.../