UN yasikitishwa na hatua ya Trump ya kuiwekea vikwazo ICC
Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa ya jana Ijumaa kuwa, vikwazo hivyo vya Washington si tu vitaathiri uchunguzi na kesi zilizoko kwenye mahakama hiyo, bali pia vinahujumu uhuru wa chombo hicho cha kimataifa.
Taarifa ya ofisi hiyo ya UN imebainisha kuwa, "uhuru wa ICC na jukumu lake la kufanya kazi bila kuingiliwa vinapaswa kulindwa ili mahakama hiyo iweze kutoa maamuzi sahihi pasina kushinikizwa, kuburuzwa, kutishiwa au kuingiliwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa sababu yoyote ile."
Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema, "wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa zinazolinda haki za binadamu, pamoja na familia zao wana haki ya kufungua mashitaka na kujua ukweli."
Juzi Alkhamisi Rais Donald Trump wa Marekani alisaini dikrii inayoruhusu maafisa wa ICC kuwekewa vikwazo. Dikrii hiyo inampa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani idhini ya kushirikiana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo katika kuzuia mali za maafisa wa ICC ambao wanahusika katika kuchunguza jinai za kivita zilizotendwa na askari wa Marekani huko nchini Afghanistan.
ICC sanjari na kupinga hatua hiyo ya kibabe ya US, imesema vikwazo hivyo ni juhudi za hivi karibuni zaidi na zisizokuwa na mfano wake zinazofanywa na Marekani dhidi ya mahakama hiyo ya kimataifa.