HRW yaitaka Ufaransa kukomesha mienendo ya kibaguzi ya polisi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61692-hrw_yaitaka_ufaransa_kukomesha_mienendo_ya_kibaguzi_ya_polisi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa taarifa likiituhumu Polisi ya Ufaransa kuwa inaamiliana kibaguzi na raia wenye asili ya Kiarabu na Kiafrika wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 19, 2020 02:40 UTC
  • HRW yaitaka Ufaransa kukomesha mienendo ya kibaguzi ya polisi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa taarifa likiituhumu Polisi ya Ufaransa kuwa inaamiliana kibaguzi na raia wenye asili ya Kiarabu na Kiafrika wa nchi hiyo.

Ripoti iliyotolewa leo na Human Rights Watch imelitaka Jeshi la Polisi la Ufaransa kukomesha mienendo ya kibaguzi na ubaguzi wa rangi unaofanywa dhidi ya Wafaransa Waarabu na wale wenye asili ya Afrika. 

Ripoti hiyo ambayo imetegemea uchunguzi uliofanyika katika miji ya  Paris, Strasbourg, Lille na Grenoble imesema kuwa, polisi wa Ufaransa wamekuwa wakipekua miili ya raia weusi na Waarabu kwa sababu za kibaguzi za tofauti za kimbari au kwa dhana potofu na ya kibaguzi kwamba, uhalifu umeenea zaidi baina ya raia weusi na Waarabu. 

Human Rights Watch imetilia mkazo udharura wa kukomeshwa mienendo ya kibaguzi nchini Ufaransa. 

Ripoti ya shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu imetolewa baada ya maandamano ya siku kadhaa katika miji mbalimbali ya Ufaransa dhidi ya mienendo ya kibaguzi ya polisi ya nchi hiyo dhidi ya Wafaransa wenye asili ya Afrika. 

Wakazi wa jiji la Paris na miji walifanya maandamano wiki iliyopita wakipinga ukatili wa polisi na ubaguzi unaoendelea kufanyika nchini humo dhidi ya raia weusi, na vilevile kupinga mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu wa Marekani dhidi ya raia mwenye asili ya Afrika wa nchi hiyo, George Floyd.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi na dhulma dhidi ya Waafrika nchini Ufaransa yalifanyika kufuatia mauaji ya raia mweusi wa nchi hiyo, Adama Traoré. Wafaransa wengi wanaamini kuwa mauaji ya raia huyo yanafanana sana na yale ya George Floyd.