Aug 02, 2020 02:23 UTC
  • Indhari ya Pompeo kwa Russia na madai ya kuondoka wanajeshi wa Marekani Afghanistan ifikapo Mei 2021

Rais Donald Trump wa Marekani ameanzisha rasmi mchakato wa kuondoka wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan kabla ya wakati ulioainishwa awali, kwa kuzingatia ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi na mapatano iliyofikia Marekani na kundi la Taliban mwezi Februari mwaka huu. Hivi sasa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani anazungumzia kuainishwa wakati wa kukamilisha mchakato huo wa kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan na wakati huo huo anatoa vitisho kwa Russia.

Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amesisitiza kuwa kwa mujibu wa mapatano ya Doha jeshi la Marekani litakuwa limeshaondoka Afghanistan ifikapo mwezi Mei mwakani. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amebainisha kuwa: "Sisi na Taliban tumesaini mapatano; na wanajeshi walioko Afghanistan hawatobakia hata mmoja. Tutawaondoa wanajeshi wetu huko. Kuna uwezekano hilo likajiri mwezi Mei 2021". Inaonekana kuwa matamshi haya ya Pompeo ni jibu kwa daghadagha kuu za Kongresi ya Marekani kuhusu hali inayowakabili wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan. Trump ametaka kuondoka awamu kwa awamu wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan katika fremu ya utekelezaji wa mapatano yaliyofikiwa  kati ya Marekani na kundi la Taliban; na mchakato huo umeshaanza kitambo nyuma. Pamoja na kuwa , wanajeshi wa Marekani walikuwa na fursa ya kuanza kuondoka Afghanistan kuanzia mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa kati ya nchi yao na kundi la Taliban lakini Washington ilishaanza siku kadhaa zilizopita mchakato wa kupunguza vikosi vyake huko Afghanistan. Kwa mujibu wa mapatano hayo, imepangwa kuwa katika kipindi cha miezi 18 Marekani iwaondoe wanajeshi wake huko Afghanistan ili kufikiwa moja ya masharti makuu ya Taliban kwa ajili ya kurejesha amani nchini humo. Hata kama kundi ya Taliban limesitisha mashambulizi yake dhidi ya vikosi ajinabi vilivyoko Afghanistan baada ya kusaini mapatano ya Februari 29 huko Doha, lakini pamoja na hayo kundi hilo limezidisha mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Kiafghani. Taliban inadai kuwa hakuna serikali nchini Afghanistan; na suala la kusitisha vita na Marekani halivijumuishi vikosi vya Afghanistan. Kwa msingi huo, kuna haja ya kufikiwa mapatano mengine nao ili kusitisha mapigano. Suala hilo limepelekea kuendelea mashambulizi ya Taliban dhidi ya vikosi vya Afghanistan na serikali ya nchi hiyo pia linaamini kuwa hicho ni kikwazo katika kutekeleza awamu nyingine ya mapatano kati ya Marekani na Taliban. Pamoja na hayo, Marekani ambayo kwa karibu miaka ishirini sasa imekwama kwenye kinamasi huko Afghanistan kivitendo haijatilia maanani pakubwa kadhia hii; na imeendeleza mchakato wa kuwaondoa wanajeshi wake katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita bila ya kuzingatia hali ya mambo na mazingira ya kiusalama. Aidha kwa kuzingatia matamshi ya Pompeo Marekani imekusudia kukamilisha mchakato huo ifikapo Mei mwakani. 

Wapiganaji wa kundi la Taliban 

Bill Rajiv mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa India anasema: "Taliban inatambua kuwa, mapatano iliyoyafikia na Marekani ni mapatano ya kuhitimisha ukaliaji mabavu. Marekani inataka kuondoka Afghanistan na imesalimu amri mbele ya matakwa yote ya Taliban." 

Suala jingine alilolieleza Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Marekani lilikuwa ni kuhusu nafasi ya Russia huko Afghanistan. Pompeo amedai kuhusu kile alichokiita pendekezo la Russia la kutoa bakhshishi kwa kundi la Taliban kwa ajili ya kuwaua wanajeshi wa Marekani na akaeleza kuwa: Sisi tumeitahadharisha Russia kuwa hatukubali kitendo cha kuibua vitisho dhidi ya usalama wa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan. Inaonekana kuwa viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani wanafanya kila linalowezekana kuituhumu Russia kuwa inaingilia masuala ya Afghanistan; na khususan ushirikiano wa Moscow na kundi la Taliban kwa ajili ya kuwauwa wanajeshi wa Marekani na kwa njia hiyo kupata sababu ya kutetea kushindwa kwao nchini humo. Msimamo huu dhidi ya Russia umebainishwa katika hali ambayo wabunge katika Kongresi ya Marekani pia wametaka kushadidishwa hatua dhidi ya Moscow khususan kuiwekea vikwazo kwa kuwepo madai ya Moscow kutoa bakhshishi ili Taliban iwaue wanajeshi wa Marekani.  Hii ni katika hali ambayo, baada ya kufikiwa mapatano kati ya Marekani na Taliban; hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyeuliwa na Taliban kuanzia mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa na idadi ya wanajeshi wa Marekani imepunguzwa kutoka elfu 13 hadi 8,600. Wakati huo huo, madai hayo yote yamekabiliwa na jibu hasi na kanusho kali la Taliban na Russia na hata Trump mwenyewe. Trump amesema kuwa yeye na washauri wake wa karibu hawana taarifa yoyote kuhusu ripoti hizo zinazohusiana na madai ya kushambuliwa mwaka uliopita wanajeshi wa Marekani   huko Afghanistan kwa uungaji mkono wa Russia. 

Wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan  

Russia inadhani kwamba lengo kuu la watoaji madai hayo ni kutaka kuharibu kadiri inavyowezekana uhusiano wa Moscow na Washington na pia kupata kisingizio kipya ili Marekani ishadidishe mashinikizo dhidi ya Russia; na wakati huo huo hiyo ni kampeni ya Wademocrat ya kuichafua haiba yaTrump katika muda huu uliosalia hadi kufanyika uchaguzi wa rais huko Marekani mwezi Novemba mwaka huu kwa kutaka aonekane kuwa ni kikaragosi cha Russia. 

Zamir Kabulov Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia Katika Masuala ya Afghanistan anasema: "Moscow inafahamu kuwa ripoti za vyombo vya habari kuhusu madai ya pendekezo la kupatiwa fedha Taliban ili iwaue wanajeshi wa Marekani ni sehemu ya porojo za kisiasa ndani ya Marekani. Hii ni kwa sababu pande zinazopendelea uwepo wa wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan zinastafidi na taarifa za uwongo ili kuhalalisha kufeli kwao huko Afghanistan."

 

 

 

 

 

 

 

Tags