Wamarekani waliowengi wamechukizwa na mdahalo baina ya Biden na Trump
(last modified Wed, 30 Sep 2020 07:20:05 GMT )
Sep 30, 2020 07:20 UTC
  • Wamarekani waliowengi wamechukizwa na mdahalo baina ya Biden na Trump

Asilimia 69 ya Wamarekani wamechukizwa na mdahalo wa kwanza wa Donald Trump na Joe Biden, wagombea wawili wa urais katika uchaguzi utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Baada ya mdahalo huo wa Biden wa chama cha upinzani cha Democrat na Trump wa chama tawala cha Republican, asilimia 69 ya Wamarekani walioutazama mdahalo huo wamesema walichukizwa na yaliyojiri. Aidha waliowengi wamesema Biden atakuwa mshindi katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Novemba 3.

Aghalabu ya vyombo vya habari na wachambuzi wa kisiasa wameutaja mdahalo huo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kuwa mdahalo ambao haukuwa na thamani na ambao unaibua wasi wasi kuhusu mustakabali wa Marekani.

Mdahalo wa Biden na Trump

Mdahalo huo ambao ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Case Western Reserve Cleveland, Ohio uligeuka na kuwa jukwaa la  shutuma, tuhuma na kufokeana. Kufuatia mdahalo huo wengi wamezidi kuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa uchaguzi wa mara hii Marekani kumalizikia kwa machafuko, hasa endapo Trump atashindwa na kukataa kukabidhi madaraka. 

Uchunguzi wa maoni katika miezi ya hivi karibuni unaonyesha kuwa, Biden anaongoza. Usimamizi mbovu wa janga la corona, ufisadi wa kimaadili wa Trump na ukandamizaji wa maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi ni kati ya sababu ambazo zimechangia kupungua kwa kiasi kikubwa umashuhuri wa rais Trump.

Tags