'Kanisa la Uingereza limefeli kukabili visa vya kudhalilishwa kingono watoto'
Ripoti ya Tume ya Uchunguzi imefichua kuwa, Kanisa la Uingereza lilifeli kuwalinda watoto wadogo dhidi ya vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kingono kwa miongo kadhaa.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana Jumanne na Tume Huru ya Uchunguzi wa Ukatili wa Kingono (IICSA) imefichua namna uozo huo wa kunajisiwa na kudhalilishwa kiongoni watoto ndani ya kanisa hilo ulivyofumbiwa macho kwa miongo mingi kwa hofu ya kupoteza hadhi taasisi hiyo ya kidini.
Profesa Alexis Jay, Mwenyekiti wa tume hiyo amesema Kanisa la Uingereza kwa miongo kadhaa limejenga utamaduni wa kutowaanika wahusika wa vitendo hivyo (vya ubakaji) na kuwazidishia machungu wahanga wa uozo huo.
Amesema kanisa hilo linapaswa kubadilisha mienendo hiyo ya kuwakingia kifua wabakaji ndani ya taasisi hiyo ya kidini, ili kuandaa mazingira kwa waathiriwa wa vitendo hivyo viovu kujitokeza wazi na kushtaki, ili waanze mara moja safari ya kuponya makovu ya kimwili na kisaikolojia walioachwa nayo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wachungaji 390 au viongozi wengine walioaminika wa Kanisa la Uingereza ambalo ni chimbuko la madhehebu ya Kianglikana duniani na lililoasisiwa mwaka 1534 baada ya kujitenga na Kanisa Katoliki, walishtakiwa kwa kuwanajisi watoto wadogo kuanzia miaka 1940 hadi 2018.

Februari mwaka jana, Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani alikiri kuwa kanisa hilo pia linakabiliwa na mgogoro wa udhalilishaji wa kingono, huku makasisi na maaskofu wa kanisa hilo wakiwafanya watawa watumwa wa ngono.
Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi na viongozi wengine wa kanisa hilo, ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki duniani.