Kundi la G77 na China zataka Iran iondolewe vikwazo mara moja
Kundi la nchi 77 (G77) pamoja na China zimetaka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viondolewa haraka iwezekanavyo.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la G77 na China wametoa mwito huo katika tangazo la pamoja lililotolewa jana Ijumaa katika Mkutano wa 44 wa kila mwaka mjini Washington.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa kundi hilo wamesema wanapinga vikali hatua za upande mmoja za kuliwekea taifa la Iran vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vimekuwa na taathira hasi katika maendeleo na ustawi wa wananchi wa nchi hiyo.
Kadhalika nchi wanachama wa Kundi la G77 pamoja na China zimetangaza kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zikisisitiza kuwa, mapatano hayo ya kimataifa ni mfano hai unaoonyesha kuwa diplomasia na mazungumzo ya pande kadhaa ndiyo njia bora ya kutatua migogoro mbali mbali duniani.
Kundi la nchi 77 lilianzishwa tarehe 15 mwezi Juni mwaka 1964 na mataifa 77 kutoka nchi zinazoendelea ambazo zilitia saini azimio la pamoja la nchi 77 zinazostawi.
Kwa sasa kundi hilo lenye nafasi kubwa katika masuala nyeti ya kimataifa ndani ya Umoja wa Mataifa lina nchi wanachama 136.