Bangladesh yawahamishia wakimbizi Waislamu Warohingya kwenye kisiwa kisichokalika
(last modified Fri, 04 Dec 2020 07:11:57 GMT )
Dec 04, 2020 07:11 UTC
  • Bangladesh yawahamishia wakimbizi Waislamu Warohingya kwenye kisiwa kisichokalika

Serikali ya Bangladesh imeanza kuwahamisha wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar na kuwapeleka kwenye kisiwa kisichokalika cha Bhashan Char.

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakisisitiza kuwa kisiwa hicho na mahali hatari kwa kuishi wanadamu. Kisiwa cha Bhashan Char kina hali ya kimaumbile ya mawe na majabali na kila mara hukumbwa na mafuriko na pepo kali za mavumbi.

Ripoti zinaeleza kuwa wakimbizi wapato 922 Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar, wameshaondolewa kwa mabasi kutoka kambi za wakimbizi za Cox nchini Bangladesh na kupelekwa bandari ya Chattogram ili kuanzia leo wasafirishwe kwa meli za jeshi la wanamaji la Bangladesh na kupelekwa kisiwa cha Bhashar Chan.

Jeshi la wanamaji la Bangladesh limejenga maskani kwenye kisiwa hicho zenye uwezo wa kupokea wakimbizi Waislamu wa Rohingya wasiopungua laki moja.

Waislamu madhulumu wa jamii ya Warohigya

Mnamo mwezi Agosti mwaka 2017, zaidi ya Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya walikimbilia Bangladesh kunusuru maisha yao na kutafuta hifadhi kutokana na vita na mauaji ya halaiki yaliyofanywa na jeshi la Myanmar na mabudha wenyewe misimamo ya kufurutu mpaka katika eneo wanaloishi la Rakhine; na hivi sasa wanaishi kwenye kambi za wakimbizi zilizoko kwenye mpaka wa Bangladesh.

Kufuatia hujuma na mashambulio hayo ya kinyama ya mwaka 2017 ya wanajeshi wa Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya, Umoja wa Mataifa ulilitangaza jeshi la Myanmar kuwa ni mhusika wa uangamizaji kizazi na mauaji ya kimbari na jeshi baya zaidi duniani.../