Hatua mpya ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa
(last modified Fri, 19 Feb 2021 02:23:28 GMT )
Feb 19, 2021 02:23 UTC
  • Hatua mpya ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa

Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na kushadidi mashinikizo dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa unaonekana kushtadi na kuchukua mkondo mpana zaidi katika miaka ya hivi karibuni katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Hivi sasa Bunge la Ufaransa likiunga mkono utendaji ulio wa chuki dhidi ya Uislamu wa Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron limechukua hatua mpya katika uwanja huo. Bunge la Ufaransa linalojulikana kama Baraza la Taifa, Jumanne iliyopita lilipasisha sheria iliyo dhidi ya Uislamuu na Waislamu katika nchi hiyo. Wabunge 347 walipiga kura ya ndio mkabala na kura 151 za hapana katika zoezi la kuupigia kura muswada wa “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” na kuupasisha. Hata hivyo, katika hatua ya mwisho sheria hiyo inapaswa kupasishwa na Baraza la Seneti na kuwa sheria kamili.

Ndani ya sheria hiyo kuna kipengee nambari 70 ambacho kinaipa uwezo serikali ya nchi hiyo wa kufunga shule za kidini na maeneo ya ibada na kuzuia kutolewa hotuba ambazo kwa mujibu wa madai ya serikali ya Paris ni za kuchupa mipaka. Aidha makundi ya kidini yanapaswa kutangaza misaada yao inayotoka nje huku akaunti zao za benki  ni lazima zikaguliwe na kuidhinishwa

Maandamano dhidi ya misimamo ya Rais wa Ufaransa iliyo dhidi ya Uisamu

 

Pamoja na hayo yote, lakini kile ambacho kiko wazi ni kuwa, sheria hiyo inawalenga Waislamu na harakati za Kiislamu nchini Ufaransa kama misikiti na vituo vya Kiislamu. Si hayo tu, sheria hiyo inawazuia mabinti wa Kiislamu wa umri wa chini ya miaka 18 kuvaa hijabu katika maeneo ya umma.

Ukweli wa mambo ni kuwa, sheria hii inahesabiwa kuwa ni sehemu ya mjumuiko wa hatua za Rais Emmanuel Macron zenye lengo la kuunga mkono thamani za kisekulari. Macron ambaye amekuwa akidhihirisha bayana chuki zake dhidi ya Uislamu amedai kwamba, kupasishwa sheria hiyo lilikuwa jambo la dharura kwa ajili ya kusaidia thamani za Ufaransa kama usawa wa kijinsia, usekulari na kung’oa mizizi ya fikra za kuchupa mipaka.

Wakosoaji wa sheria hii iliyozusha makelele mengi na iliyo na chuki dhidi ya Uislamu wanaamini kuwa, Rais Macron na serikali  yake lengo lao hasa ni kutaka kutumia sheria hiyo kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kuuandama Uislamu na kushadidisha mashinikizo ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini humo.

Maandaano ya kulaani chuki dhidi ya Uislamu

 

Jumapili iliyopita raia wa Ufaransa hususan Waislamu wa nchi hiyo walikusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Paris na kuandamana wakipinga mpango huo wa serikali ambao unalenga kushadidisha mibinyo na mashinikizo dhidi ya Waslamu wa nchi hiyo. Waandamanaji hao wameonya kuwa, kupasishwa sheria hiyo  kutapelekea kuwekewa mipaka  baadhi ya uhuru wa kidini nchini humo na kimsingi Waislamu ndio walengwa wakuu.

Macron amekuwa na utendaji usio wa kimantiki ambapo amekuwa akiunga mkono kwa nguvu zake zote hatua, chuki na vita dhidi ya Uislamu sambamba na kuvunjiwa heshima dini hii na matukufu yake. Mbali na Macron kufanya kila awezalo kuhakikisha kunapasishwa sheria ambayo itabinya na kuwekea mipaka Uislamu na Waislamu, kiongozi huyo amekuwa aking'ang'ania msimamo wake wa kuunga mkono hatua zilizo dhidi ya dini hii kama kuvunjiwa heshima matukufu yake kwa kisingizio eti cha uhuru wa kutoa maoni.

Mfano wa wazi katika hilo, ni hatua ya Rais wa Ufaransa ya kuunga mkono kikamilifu hatua ya gazeti la Charlie Hebdo la Ufaransa ya kuchapisha vikatuni na vibonzo vinavyomvunjia heshima Bwana Mtume SAW kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.  Hata hivyo hatua hiyo haikuwa na natija nyingine ghairi ya kuwachochea Waislamu na kuongezeka mizozo na mivutano katika jami ya Ufaransa.

Miito ya kususia bidhaa za Ufaransa imdeendelea kutolewa baada ya vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu kushadidi katika nchi hiyo ya bara Ulaya

 

Katika radiamali yake kwa vitendo dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa, Rais Macron ameyafanya matukio hayo kama wenzo wa kufikia malengo yake na kulifanya hilo kama kisingizio cha kuwatwisha zaidi Waislamu mibinyo na hatua za kuwakandamiza.

Masoud Shajareh, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kimataifa ya Haki za Binadamu za Kiislamu (IHRC) yenye makao yake mjini London Uingereza anasema kuwa, Rais Macron amekuwa akiuandama kwa makusudi  Uislamu hasa pale aliposema kwamba, dini hii inakabiliwa na mgogoro. Rais huyo amelazimika kushikamana na misimamo ya ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu kwa kiwango kikubwa kuliko hata huko nyuma, ili kwa njia hiyo aweze kuyaridhisha makundi yenye misimamo ya kufurutu ada ya mrengo wa kulia yampgie kura katika uchaguzi ujao.

Hivi sasa inatarajiiwa kuwa, kupasishwa “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” ambayo itapelekea kuibuka mashinikizo na mibinyo zaidi dhidi ya Waislamu wa Ufaransa, kutapelekea Waislamu hao wajitokeze na kutoa radiamali dhidi ya hatua hiyo.