Kuendelea Azerbaijan kununua silaha za utawala haramu wa Israel
Licha ya kufikia tamati vita vya Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia kuhusu umiliki wa eneo la Karabakh na kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya pande mbili kwa upatanishi wa Russia, lakini kumeanza duru mpya ya kununua silaha za utawala haramu wa Israel unaofanywa na serikali ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan.
Kuhusiana na hili, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stokholm (SIPRI) imetangaza katika ripoti yake kwamba: Jamhuri ya Azerbaijan imenunua asilimia 69 ya silaha na zana zake za kijeshi inazohitajia kutoka kwa utawala ghasibu wa Israel
Hii ni katika hali ambayo, katika miaka ya kati ya 2016 hadi 2020, Jamhuri ya Azerbaijan ilinunua asilimia 17 tu ya silaha zake kutoka Russia. Serikali ya Rais Ilham Aliyev inanunua silaha kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Israel na kupanua uhusiano wake na utawala huo katika hali ambayo, wananchi Waislamu wa Azerbaijan wameendelea kupinga vikali nchi yao kuwa na ushirikiano na utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa makubaliano mapya, katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali ya Rais Aliyev itaingiza nchini humo kutoka Israel silaha za kisasa zenye thamani ya dola bilioni mbili. Katika mkataba uliotiwa saini baina ya viongozi wa serikali ya Azerbaijan na utawala bandia wa Israel, imeafikiwa kuwa, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Israel itakuwa mdhamini na muandaaji wa silaha za kisasa za Azerbaijan. Miongoni mwa silaha hizo ni pamoja na makombora aina ya cruise na ndege za mashambulio zisizo na rubani (drone).
Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, silaha za Azerbaijan ilizonunua kutoka kwa utawala vamizi wa Israel zinajumuisha ndege zisizo na rubani, zana za kijasusi na makombora ya balestiki, huku akthari ya manunuzi yake kutoka Russia yakihusu magari ya kijeshi na suhula za mizinga.
Kuna ukweli ambao unafumbiwa macho na vyombo vya habari wa Azerbaijan na vya kieneo kuhusiana na ununuzi wa silaha wa serikali ya Baku kutoka Israel nao ni Tel Aviv kuitumia vibaya serikali ya Rais Ilham Aliyev. Ukweli wa mambo ni kuwa, awali utawala wa kibaguzi wa Israel unaiuzia Azerbaijan silaha na zana za kijasusi na baada ya muda huilazimisha nchi hiyo kutumia silaha hizo hizo dhidi ya maslahi ya nchi ya tatu hususan Iran na Russia.
Rob Gaurik, mtaalamu, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kiuchumi na kisiasa katika ubalozi wa Marekani mjini Baku, alitangaza mwaka 2009 katika ripoti ya kidiplomasia kwamba: Lengo kuu la Israel ni kuibadilisha Jamhuri ya Azerbaijan na kuifanya kuwa medani ya kufanyia ujasusi na soko la zana za kijeshi dhidi ya Iran na katika uga wa kieneo kwa ujumla.
Kueneza ripoti kama hizi ni ishara ya wazi kwamba, daima utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiitumia serikali ya Rais Ilham Aliye wa Azerbaijan dhidi ya maslahi ya kitaifa ya nchi zenye kujitawala na zisizokubali kuburuzwa katika eneo hili.
Katika fremu hiyo, katika miaka ya hivi karibuni, utawala ghasibu wa Israel umefanya juhudi maradufu kwa ajili kupenya na kuwa na ushawishi katika nchi kama Azerbaijan na nchi nyingine za Asia ya Kati na Caucasia. Hatua hizo zimefuatiwa na kuzusha machafuko na mapigano baina ya nchi hizo.
Ya’aqub Qedami, mchambuzi wa Kizayuni amesema katika mahojiano aliyofanyiwa kuhusiana na mustakabali wa Armenia kwamba: Kuna uwezekano mkubwa mno wa Armenia kufutwa katika ramani ya dunia katika mustakabali kutokana na siasa zilizochaguliwa na wenye vipawa wa nchi hiyo na matokeo yake kuwa ni kuibuka uhakika mpya kwa mara nyingine katika mipaka ya Caucasia ambao utakuwa ni maslahi ya wahusika amilifu katika uwanja huo.
Matamshi haya ya uingiliaji mambo ya mchambuzi huyu wa Israel yanaonyesha kwamba, utawala huo wa kibaguzi umekuwa ukitumia kila njia kwa ajili ya kufikia malengo na matakwa yake.
Kuhusiana na hilo, madhali Jamhuri ya Azerbaijan na serikali yake inayoongozwa na Rais Ilham Aliyev itaendelea kudhamini maslahi ya Israel, basi itasalimika na vitisho vya utawala huo wa kibaguzi. Kinyume na hivyo, Jamhuri ya Azerbaijan nayo itakabiliwa na vitisho vya utawala haramu wa Israel.