Baada ya China kuiwekea vikwazo UK, sasa London yalalamika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i68336-baada_ya_china_kuiwekea_vikwazo_uk_sasa_london_yalalamika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amelalamikia vikali vikwazo vilivyowekwa na China dhidi ya nchi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2021 22:02 UTC
  • Baada ya China kuiwekea vikwazo UK, sasa London yalalamika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amelalamikia vikali vikwazo vilivyowekwa na China dhidi ya nchi yake.

Dominic Raab, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alisema jana Ijumaa kwamba vikwazo vya China dhidi ya nchi yake ni uvunjaji wa haki za binadamu.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uingereza pia amesema, serikali ya China imeamua kuwawekea vikwazo wanaoikosoa Beijing.

Matamshi hayo yamekuja baada ya China kuamuua kujibu kivitendo vikwazo ilivyowekewa na nchi za Magharibi. Jana Ijumaa, China iliwawekea vikwazo maafisa 9 na taasisi 4 za Uingereza kutokana na kueneza uongo na kupotosha walimwengu kuhusu hali ya eneo la Xinjiang la magharibi mwa China.

Waislamu wa jamii ya Uyghur nchini China

 

Wakati inatangaza vikwazo hivyo dhidi ya Uingereza, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema kuwa, vikwazo hivyo vinawahusu maafisa hao 9 wakubwa wa Uingereza na familia zao ambao wamepigwa marufuku kutia mguu wao katika ardhi ya China. Aidha raia wote wa China na taasisi za nchi hiyo zimepigwa marufuku kushirikiana na kufanya muamala wowote na maafisa hao 9 wa Uingereza na familia zao.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Beijing ina haki ya kuchukua hatua kubwa zaidi katika uwanja huo.

Jumatatu wiki hii, Umoja wa Ulaya pamoja na Uingereza ziliiwekea vikwazo China kwa madai ya kuvunjwa haki za binadamu za watu wa jamii ya Uyghur.

Mara kwa mara China imekuwa ikikanusha madai ya kuvunja haki za jamii ya wachache ya Uyghur na kudai kuwa suala hilo linatumiwa kisiasa na maadui.