Amnesty: China imewafanyia Waislamu wa Uighur 'jinai dhidi ya binadamu'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i71134-amnesty_china_imewafanyia_waislamu_wa_uighur_'jinai_dhidi_ya_binadamu'
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema Waislamu wa jamii ya Uighur nchini China wanakabiliwa na vitendo vya mateso na unyanyasi unaoelezwa kuwa umekuwa ukifanywa na serikali ya Beijing, na kusisitiza kuwa dhulma hizo zina uzito wa 'jinai dhidi ya binadamu.'
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2021 03:22 UTC
  • Amnesty: China imewafanyia Waislamu wa Uighur 'jinai dhidi ya binadamu'

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema Waislamu wa jamii ya Uighur nchini China wanakabiliwa na vitendo vya mateso na unyanyasi unaoelezwa kuwa umekuwa ukifanywa na serikali ya Beijing, na kusisitiza kuwa dhulma hizo zina uzito wa 'jinai dhidi ya binadamu.'

Ripoti ya kurasa 160 ya Amnesty iliyotolewa jana Alkhamisi inajumuisha ushahidi wa baadhi ya Waislamu wa jamii ya Uighur waliokuwa wanazuiliwa na vyombo vya usalama vya Beijing katika jimbo la Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnès Callamard amesema jamii ya Waislamu walio wachache ya Uighur wanapitia mateso makali, jinai dhidi ya binadamu na ukiukaji mwingine wa kutisha wa haki za binadamu tokea mwaka 2017, na kwamba jinai hizo zinapaswa kuishtua jamii ya mwanadamu. 

Ripoti hiyo mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International imesema, baadhi ya wanawake Waislamu wa jamii ya Uighur nchini China walifanyiwa vitendo visivyo vya kibinadamu kama mateso na kubakwa, walipokuwa wakishikiliwa katika kambi mbalimbali kwa miezi kadhaa.

Maafisa usalama wa China wanavyoamiliana na Waislamu wa Uighur

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni moja wa jamii ya Uighur ya Waislamu walio wachache wanashikiliwa kama mahabusu katika kambi za 'marekebisho' katika fremu ya kampeni eti ya kupambana na misimamo mikali. Asasi mbalimbali zimekuwa zikilaani katika ripoti zao ukandamizaji huo mkubwa unaofanywa na serikali ya China dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur katika jimbo la Xinjiang kaskazini mwa China.

Hata hivyo serikali ya China imekuwa ikikana mara kwa mara tuhuma dhidi yake za mateso dhidi ya Waislamu, ikisema kuwa inawapatia mafunzo katika kambi ili waondokane na fikra za itikadi kali. Wauighur wanaishi kaskazini magharibi mwa China katika jimbo lenye mamlaka yake ya ndani la Xinjiang.