Oxfam: Dunia inakabilwa na mgogoro wa baa la njaa
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limetangaza kuwa, watu 11 hufariki dunia kila baada ya dakika moja kote duniani kutokana na njaa.
Ripoti ya Oxfam imesema kuwa idadi ya watu wanaoishi katika mazingira yanayoshabihiana na ya baa la njaa imeongezeka mara sita katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la "Virusi vya Njaa Kuongezeka Maradufu", Oxfam imeandika kuwa, idadi ya watu wanaouawa na njaa duniani ni kubwa zaidi kuliko ya wale wanaofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 ambayo inaua karibu watu saba kwa kila dakika moja kote duniani.
Shirika hilo limetangaza kuwa, kwa sasa watu milioni 155 kote duniani wanasumbuliwa na mgogoro wa njaa, kiwango ambacho inasema kimeongezeka kwa asilia 20 ikilinganishwa na mwaka jana.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa karibu thuluthi mbili ya watu hao wanaosumbuliwa na baa la njaa wanaishi katika nchi zilizoathiriwa na vita.

Ongezeko la joto duniani na athari mbaya za kiuchumi zilizosababishwa na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona pia vimesababisha ongezeko la asilimia 40 ya bei za chakula ulimwenguni. Imesema ongezeko hilo la bei za vyakula limewatumbukiza mamilioni ya watu katika njaa na uhaba wa chakula.