NATO: Ikiwa Taliban itaidhibiti Afghanistan kwa njia ya kijeshi haitatambuliwa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i73488-nato_ikiwa_taliban_itaidhibiti_afghanistan_kwa_njia_ya_kijeshi_haitatambuliwa_kimataifa
Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO ametangaza kuwa, ikiwa kundi la Taliban litaidhibiti Afghanistan yote kupitia mashambulio yake ya kijeshi halitatambuliwa kimataifa.
(last modified 2026-02-15T05:39:07+00:00 )
Aug 14, 2021 07:44 UTC
  • NATO: Ikiwa Taliban itaidhibiti Afghanistan kwa njia ya kijeshi haitatambuliwa kimataifa

Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO ametangaza kuwa, ikiwa kundi la Taliban litaidhibiti Afghanistan yote kupitia mashambulio yake ya kijeshi halitatambuliwa kimataifa.

Jens Stoltenberg ameeleza hayo katika taarifa, ambapo sambamba na kudokeza kuwa, amefanya kikao cha mashauriano na nchi wanachama wa NATO kujadili hali ya Afghanistan amedai pia kwamba, shirika hilo la kijeshi litaiunga mkono serikali ya Kabul kadiri itakavyowezekana, lakini usalama wa wafanyakazi wake ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote kile.

Stoltenberg aidha amesema, ana wasiwasi juu ya vitendo vya ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Taliban na akaongeza kwamba, kundi hilo inapasa litambue kuwa ikiwa litaidhibiti Afghanistan kwa mabavu halitatambuliwa na jamii ya kimataifa, lakini kuna nia na irada ya dhati ya kuunga mkono utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nchi hiyo.

Wanamgambo wa kundi la Taliban

Katibu Mkuu huyo wa NATO amekamilisha taarifa yake kwa kusema, shirika hilo la kijeshi la madola ya Magharibi litaendelea kuwepo kidiplomasia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Wigo wa vita na mapigano nchini Afghanistan umepanuka zaidi baada ya kundi la Taliban kuanzisha mashambulio ya kuiteka miji mikuu ya majimbo ya nchi hiyo; na hadi sasa mapigano makali yangali yanaendelea kati ya vikosi vya serikali na vile vya wanamgambo wa kundi hilo, na kuifanya hali ya usalama ya Afghanistan iwe mbaya zaidi.../