Guterres: UN iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemtumia ujumbe Rais wa Iran na kusema kuwa, taasisi hiyo ya kimataifa iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu.
Katika ujumbe wake kwa Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: UN na Katibu Mkuu wake wana azma ya kufanya kazi na serikali mpya ya Iran ili kuhakikisha amani, usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu zinatawala kote duniani.
Guterres amebainisha katika ujumbe huo kwa Raisi kuwa, "Kuanza kipindi cha urais wako kumesadifiana na kipindi nyeti kwa Iran, eneo na dunia nzima kwa ujumla, na vile vile (kimeanza) wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto za pamoja kama janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi, na migogoro ya kutisha katika maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Asia Magharibi."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa, maliasili na rasilimali watu wa Jamhuri ya Kiislamu ni hazina kubwa ya kuboresha si tu maisha ya wananchi wa Iran bali pia ya watu wengine katika pembe nyingine za dunia.
Sayyid Ebrahim Raisi alishinda uchaguzi wa rais wa mwezi Juni mwaka huu, kwa kupata zaidi ya kura milioni 17 na laki tisa.