Tanzania, Kenya na Afrika Kusini zaanza kununua gesi asilia ya Iran
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza kuziuzia nchi za Afrika Kusini, Kenya na Tanzania gesi asilia oevu (LNG).
Esmaeel Hasham Firouz, Mkurugenzi wa Mahuruji na Maduhuli wa Shirika la Taifa la Kusambaza Bidhaa za Mafuta la Iran amesema tayari Iran imeanza kusafirisha kwa njia ya bahari gesi hiyo kwenda katika nchi tatu hizo za Afrika.
Ofisa huyo amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliuza nje ya nchi tani 127,000 za gesi asilia mwaka jana na kwamba kiwango hicho kinatazamiwa kuongezeka mwaka huu, haswa baada ya kuondolewa vikwazo taifa hili.
Hii ni katika hali ambayo, kampuni ya Ujerumani ya Linde tayari imakubaliana na Iran kukamilisha miradi ya mashirika ya LNG Pars na LNG Persian ya nchi hii. Mashirika ya Royal Dutch Shell ya Uholanzi, Repsol ya Uhispania na Total ya Ufaransa yalisitisha miradi hiyo mwaka 2011, baada ya Iran kuwekewa vikwazo vya kidhalimu. Mashirika hayo yalitakiwa kuzalisha tani milioni 40 ya gesi kila mwaka kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.
Iran ina hifadhi ya mita mraba bilioni 187 za gesi asilia katika Ghuba ya Uajemi ambapo hivi sasa ina uwezo wa kuchimba asilimia 75 ya gesi hiyo. Inakadiriwa kuwa Iran ni nchi ya pili duniani kwa hifadhi ya gesi baada ya Russia, jambo ambalo linaifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa moja ya nchi muhimu duniani katika sekta ya mafuta na gesi na hivyo kuendelea kuvutia mashirika makubwa ya kimataifa.