Nov 12, 2021 10:55 UTC
  • Wanajeshi 30,000 wa Marekani wamejiua tokea mwaka 2001

Tokea Septemba 11 mwaka 2001 hadi sasa, zaidi ya wanajeshi 30,000 wa Marekani wamejiua. Hayo yamedokezwa na Cori Bush mbunge wa chama tawala cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani.

Katika ujumbe wa Twitter kwa mnasaba wa Siku ya Maveterani wa Kivita, Bush amesema,  "baada ya Septemba 11 mwaka 2001 hadi sasa zaidi ya wanajeshi 30,000 wa Marekani wamejiua. Mbali na hayo, maveterani wa kivita wapatao 40,000 hawana nyumba."

Idadi ya askari wa Marekani wanaojiua wakiwemo maveterani wa kivita imeongezeka sana katika muongo mmoja uliopita na ni zaidi ya idadi ya askari wote wa Marekani waliouawa katika vita vya Iraq, Afghanistan na Vietnam.

Idara ya Maveterani wa Kivita ya Marekani inasema visa vya kujiua miongoni mwa maveterani vimeongezeka sana kiasi kwamba mwaka 2019 maveterani 17 walikuwa wanajiua kila siku.

Veterani wa kivita Marekani akiomba msaada barabarani

Hivi karibuni Ikulu ya Rais wa Marekani ilitangaza muongozo kuhusu hatua za kuchukuliwa ili kuzuia visa vya kujiua miongoni mwa askari wa nchi hiyo.

Gazeti la New York Times limechapisha ripoti inayobaini kuwa pamoja na kuwepo jitihada za juu chini ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, lakini idadi ya askari wanaojiangamiza nchini humo inazidi kuongezeka.

Tags