Feb 27, 2024 12:42 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Dhamiri zilizoamka zinapinga mauaji ya kimbari ya Wapalestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amekitaja kilio cha rubani wa Marekani aliyejitoa mhanga kwa kujichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington akipinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza kuwa ni sauti kubwa ya dhamiri zilizoamka nchini Marekani zinazopinga uungaji mkono wa serikali nchi hiyo kwa mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Ni baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kutangaza jana (Jumatatu) kwamba rubani wa Jeshi la Anga la nchi hiyo, Aaron Bushnell, aliyejichoma moto mbele ya Ubalozi wa Israel mjini Washington akipinga vita katika Ukanda wa Gaza, amefariki dunia.

Kabla ya kujichoma moto akiwa amevalia sare za kijeshi, rubani huyu wa Marekani alitangaza kwenye video mubashara kwamba hatashiriki tena katika mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumzia tukio hilo, Nasser Kanani msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika kwenye mtandaoni wa X kwamba: Kujichoma moto kwa Aaron Bushnel," afisa wa Jeshi la Anga la Marekani akipinga jinai zinazoendelea kufanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza, kumeonesha ni kiwango gani dhamiri zilizoamka huko Marekani zinavyoaibishwa na uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo kwa mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Kilio cha Bushnell ni sauti kubwa ya dhamiri zilizoamka nchini Marekani dhidi ya himaya na uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inaonesha kuwa, kabla ya kujitia moto, askari huyo wa Marekani alisikika akisema "Sitashiriki tena katika mauaji ya kimbari" huku akipaza sauti na kusema "Palestina Huru."

Tags