Maoni: Wamarekani wanaamini Israel imefanya mauaji ya kimbari Gaza
Nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa, kumefanyika mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika Marekani ambapo nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa, asilimia 50 ya Wamarekani walioshiriki katika uchunguzi huo wa maoni walisema kwa uhakika kabisa kwamba, Israel inafanya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Aidha washiriki wengine walisema kuwa, kuna uwezekano Israel ikawa inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza.
Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yametangazwa katika hali ambayo, wananchi wa Marekani wamekuwa wakiandamana mara kwa mara wakipinga uungaji mkono na himaya ya serikali ya Washington kwa jinai na mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutaka kusitishwa mara moja vita huko Palestina.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, karibu Wapalestina 28,000 wameuawa shahidi, na wengine zaidi ya 67,000 wamejeruhiwa na wanajeshi katili wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel huko Gaza.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa zaidi ya Wapalestina milioni moja wanatangatanga bila makazi katika mitaa ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Katika upande mwingine, Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amezitaka nchi zilizositisha msaada wa kifedha kwa shirika hilo kufikiria upya uamuzi wao.