Putin akosoa hujuma dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi
(last modified Fri, 24 Dec 2021 15:55:16 GMT )
Dec 24, 2021 15:55 UTC
  • Putin akosoa hujuma dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

Rais wa Russia amekosoa hatua za kuhujumu na kupiga ita Uislamu na matukufu ya din hiyo katika nchi za Magharibi.

Vladimir Putin aliyekuwa akizungumza na waandishi habari mjini Moscow amekosoa hatua ya karibuni ya kuujumu Uislamu katika nchi za Magharibi na kusema kuwa, kuuvunjia heshima Uislamu na Mtume Muhammad (saw) si sehemu ya uhuru wa kusema na kujieleza.

Rais wa Russia ameongeza kuwa, hujuma ya karibu dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi inaweza kuchochea chuki na misimamo mikali.

Chuki dhidi ya Uislamu na unyanyasaji wa maneno na wa kimwili dhidi ya Waislamu vimeongezeka sana huko Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kukua kwa kasi makundi na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na kuzidi ushawishi wa wanasiasa wenye siasa kali.

Kwa ujumla, hujuma na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi vinafanywa kupitia vitendo kama kuwafungulia kesi bandia Waislamu, kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu na propaganda hasi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mfano wa karibuni zaidi ni uchapishaji wa vibonzo vinavyomkashifu na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).