Wajapan waandamana kulaani ziara ya Rais wa Marekani Hiroshima
Maelfu ya wananchi wa Japan wameandamana kulaani kitendo cha Rais Barack Obama wa Marekani cha kukataa kuomba radhi kwa jinai zilizofanywa na nchi yake za kuishambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki ya nchi hiyo.
Maandamano hayo yamefanyika huku Rais wa Marekani akitembelea moja ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya na jinai hiyo ya Marekani huko Japan, jana Ijumaa. Obama amefuatana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe kwenye ziara hiyo.
Rais huo wa Marekani amekataa kuwaomba radhi wananchi wa Japan kwa jinai za kutisha zilizofanywa na nchi yake za kuishambulia kwa mabomu angamizi ya atomiki miji hiyo ya Japan na kuua watu wanaokadiriwa 140,000 kwa mkupuo mmoja katika mji wa Hiroshima pekee. Jinai hiyo ya Marekani ilifuatiwa na jinai nyingine ya shambulio la atomiki katika mji wa bandari wa Nagasaki na kuua watu wapatao 70,000 wasio na hatia.
Rais wa Marekani ametoa mwito wa kuangamizwa silaha za nyuklia duniani katika hali ambayo nchi hiyo ya kibeberu inaendelea kujilimbikizia silaha za kisasa kabisa za nyuklia. Ripoti zinaonesha kuwa, Marekani ina silaha zipatazo 2,000 za nyuklia ambazo ziko tayari kufyatuliwa wakati wowote ule na kusababisha maangamizi makubwa duniani.