Ufaransa imeanzisha uchunguzi kuhusu Mkuu wa Interpol raia wa Imarati
Baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani kufichua hadharani jinai zinazofanywa na Mkuu wa Polisi ya Kimataifa (Interpol) ambaye ni raia wa Imarati; Idara ya Mahakama nchini Ufaransa imeanzisha uchunguzi kuhusu afisa huyo wa Intepol.
Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa, maafisa wa mahakama nchini Ufaransa tayari wameanzisha uchunguzi kuhusu Ahmed Nasser Al Raisi Mkuu wa Interpol ambaye ni raia wa Imarati aliyechaguliwa hivi karibuni kushikilia wadhifa huo licha ya tahadhari za mashirika ya kutetea haki za binadamu kuhusu afisa huyo.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Ufaransa ya kupambana na ugaidi imeanzisha uchunguzi wa awali kuhusu mkuu huyo wa Interpol kufuatia malalamiko kutoka kwa mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali. Imeelezwa kuwa, mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali yanamtuhumu Al Raisi kuwa aliwatesa wapinzani nchini Imarati wakati alipokuwa akihudumu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.
Malalamiko yaliyowasilishwa na Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Al-Khalij yanaeleza kuwa, Mkuu wa Interpol alimtesa na kumfanyia vitendo vya kikatili Ahmed Mansoor mpinzani wa utawala wa Imarati ambaye amekuwa akishikiliwa katika seli ya peke yake bila ya kuonana na wafungwa wengine huko Imarati kwa miaka minne sasa. Vilevile anashtakiwa kwa tuhuma za kutenda jinai nyingine dhidi ya binadamu.
Viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wanasema kuwa, Ahmed Mansoor ambaye alitiwa nguvuni mwaka 2017 amehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kwa tuhuma za kuwakosoa viongozi wa nchi hiyo kwa kukiuka haki za binadamu na kile lilichotajwa kuwa kuchafua taswira ya Imarati mitandaoni.
