Wanazuoni Uingereza walaani filamu inayouvunjia heshima Uislamu
Wanazuoni wa Kiislamu nchini Uingereza wamelaani na kukosoa vikali filamu tata ya "Mwanamke wa Peponi" yenye kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.
Maulamaa hao walikusanyika jana Ijumaa katika mji wa Birmingham, kuilaani filamu hiyo tata, wakati huu ambapo maandamano ya nchi nzima yanaendelea kushuhudiwa nchini humo kutaka filamu hiyo ipigwe marufuku na isirushwe tena hewani.
Taarifa ya pamoja ya wanazuoni hao wakiwemo wa Kishia, Kisunni na Kisufi imeieleza filamu hiyo kuwa mzizi wa kuibua fitina na migawanyiko ya kidini.
Filamu hiyo ambayo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mnamo Juni 3, imeibua ghadhabu miongoni mwa Waislamu katika nchi mbalimbali duniani.

Mwaka jana pia, wanazuoni wa Kishia na maulamaa wa madhehebu nyingine za Kiislamu nchini Pakistan walisisitiza kuwa, filamu hiyo inayofahamika kwa Kiingereza kama "The Lady of Heaven" inakusudia kupanda mbegu za chuki na uhasama miongoni mwa Waislamu, ili kufikia lengo la madola ya kibeberu la kuumiza hisia na nyoyo za Umma wa Kiislamu.
Walisema lengo la filamu hiyo ovu iliyotayarishwa na Yasser Al-Habibi ni kutaka kuchafua anga safi ya umoja, mshikamano, maelewano na udugu uliopo katika mataifa ya Kiislamu.