Kwa nini jamii ya kimataifa haitaki kuitambua rasmi serikali ya Taliban?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86212-kwa_nini_jamii_ya_kimataifa_haitaki_kuitambua_rasmi_serikali_ya_taliban
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan anasema: Hivi sasa, jamii ya kimataifa inaafikiana katika suala la kutoitambua rasmi serikali ya Taliban.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 24, 2022 02:24 UTC
  • Kwa nini jamii ya kimataifa haitaki kuitambua rasmi serikali ya Taliban?

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan anasema: Hivi sasa, jamii ya kimataifa inaafikiana katika suala la kutoitambua rasmi serikali ya Taliban.

Andreas von Brandt amesema kuwa serikali jumuishi na demokrasia nchini Afghanistan ndivyo vinavyohitajika kwa ajili ya kutambuliwa rasmi kundi hilo kama serikali.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan amesisitiza udharura wa kuendelezwa misaada ya jamii ya kimataifa kwa watu wa Afghanistan na kusema: Misaada hii haipaswi kupewa kundi la Taliban. Andreas von Brandt ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa Bunge la Ulaya, ameiomba jamii ya kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Afghanistan.

Brendt amesema, hivi sasa makubaliano ya jamii ya kimataifa ni kutoitambua rasmi Taliban na akasema: Hii haina maana ya kusimamisha misaada ya kimataifa kwa watu wanaohitaji msaada wa Afghanistan.

Andreas von Brandt

Matamshi hayo ya balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan yameonyesha kuwa jamii ya kimataifa, au kwa uchache nchi za Magharibi na washirika wao katika maeneo mengine ya dunia, haziko tayari kuukubali rasmi utawala wa Taliban nchini Afghanistan, na hapana shaka kuwa msimamo huu na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya utaitia wasiwasi serikali ya Taliban. Hii ni kwa sababu matamshi hayo ya Brendt yatakuwa msingi wa kutathmini utendaji wa Taliban na jinsi nchi za Magharibi zinavyopasa kuamiliana na kundi hilo.

Nchi za Magharibi, ambazo zimetangaza kuwa kigezo cha kutambuliwa rasmi utawala wa kundi la Taliban ni uundaji wa serikali jumuishi, inayoheshimu viwango vya haki za binadamu, kuheshimu uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii, na kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya jamii ya wanawake wa Afghanistan, zinaiona ripoti ya balozi wa EU katika nchi hiyo kuwa ndio msingi wa maamuzi yake ya baadaye kuhusiana na Taliban. Hata hivyo matamshi ya Brendt, yanasisitiza kuwa kutotambuliwa kundi la Taliban kusiwe na taathira mbaya katika zoezi la kupeleka misaada kwa watu wa Afghanistan, lakini misaada hiyo haipaswi kupewa serikali ya Taliban.

Licha ya matamshi ya balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan kuhusu haja ya kutenganisha mambo mawili yaani udharura wa kuendezwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Afghanistan na msimamo wa EUu kuhusu utawala wa Taliban, lakini misaada ya nchi za Magharibi kwa nchi hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ya karibuni, jambo ambalo limesababisha matatizo mengi kwa watu wa Afghanistan.

Watu wa Afghanistan wanasumbuliwa na matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii

Sayyid Javad Hosseini, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan, anasema: "Sidhani kama jamii ya kimataifa itatambua rasmi utawala wa Taliban maadamu kundi hilo halijatimiza vigezo na masharti ya jamii ya kimataifa."

Kwa kuzingatia kusitasita kwa jamii ya kimataifa katika suala hili la kuukubali rasmi utawala wa Taliban, pamoja na kupungua kwa kiasi kikubwa misaada ya kimataifa kwa Afghanistan, inatazamiwa kuwa serikali ya Taliban itakabiliwa na matatizo mengi katika kusimamia masuala ya nchi hiyo.

Msimamo wa Taliban wa kulazimisha njia na fikra ya aina moja katika kuendesha na kusimamia serikali, kuweka vikwazo vikubwa kwa jamii ya wanawake na kupuuza viwango vya haki za binadamu na matakwa ya jamii ya kimataifa ya kuunda serikali shirikishi itakayojumuisha makabila yote ya Afghanistan, imesababisha hali na mgongano kati ya kundi hilo na jamii ya kimataifa, na kuwazidishia Waafghani gharama na matatizo makubwa ya kiuchumi na kisiasa.