Waziri Mkuu wa Hungary: Vikwazo dhidi ya Russia vimefeli
Waziri Mkuu wa Hungary amekiri kuwa vikwazo shadidi vya Wamagharibi dhidi ya Russia vimefeli na kugonga mwamba, na kusisitiza kwamba serikali za nchi za Ulaya zinaporomoka.
Viktor Orban alisema hayo jana Jumamosi katika hotuba aliyoitoa huko Romania na kuongeza kuwa, "Stratejia mpya inahitajika, na inapaswa kujikita kwa mazungumzo ya amani na kuandaliwa pendekezo zuri la amani."
Orban ambaye alichaguliwa kwa kipindi cha nne mfululizo mwezi Aprili mwaka huu amesisitiza kuwa, nchi hiyo licha ya kuwa mwanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, lakini haitajiingiza katika vita vinavyoendelea katika nchi jirani ya Ukraine.
Waziri Mkuu huyo wa Haungary amekuwa akisisitiza kuwa, serikali yake haitounga mkono vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na vile vile msimamo wa EU wa kuzitaka nchi wanachama wa umoja huo kupunguza uagizaji wa gesi kutoka Russia.
Hivi karibuni, Waziri wa Fedha wa Russia alisema, kuondolewa vikwazo na Magharibi dhidi ya nchi hiyo kutapelekea kushuka bei za vyakula na nishati duniani na akafafanua kwamba, kuhusu ni kwa muda gani bei za nishati na vyakula zitaendelea kuwa za juu, hilo litategemea na muda vitakaochukua vikwazo vilivyowekwa na Magharibi.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuendelezwa sera za uadui dhidi ya Russia na nchi za Ulaya kumehatarisha pia usalama wa ndani wa bara hilo.