Russia yakamata magaidi wa ISIS, yazuia hujuma za kigaidi
Vikosi vya usalama Russia vimewakamata magaidi saba wa kundi la ISIS (Daesh) ambao walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miji kadhaa kote Russia.
Kikosi cha Polisi wa Upelelezi Russia, FSB, imetangaza kuwakamata magaidi hao wakufurishaji wakiwemo raia wa Russia na raia wengine wa nchi za katikati mwa Asia. Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax, magaidi hao wamekamatwa katika mji wa Yekaterinburg eneo la Urals. FSB imesema magaidi hao walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu Moscow na mji wa St Petersburg na pia katika eneo la Sverdlovsk huko Urals.
Taasisi hiyo ya usalama Russia imeongeza kuwa, magaidi hao walikuwa wakiongozwa na gaidi mmoja wa ISIS aliyeingia nchini humo akitokea Uturuki.
Siku chache zilizopita, Andrey Przhezdomsky, msemaji wa Kamati ya Taifa ya Russia ya kupambana na ugaidi alisema mitandao ya kigaidi yenye mfungamano na magaidi wa ISIS ilikuwa inapanga kufanya hujuma Russia na barani Ulaya.
Russia inasema mwaka 2015 iliwazuia raia wake zaidi ya 100 waliokuwa wanapanga kuondoka nchini humo kujiunga na magaidi wa ISIS. Wakuu wa usalama Russia wanakadiria kuwa, kuna magaidi kati ya 5000 hadi 7000 kutoka nchi za shirikisho la zamani la Sovieti ambao wamejiunga na magaidi wa ISIS katika nchi za Syria na Iraq.
Tokea Septemba 30 mwaka jana, Russia imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya ISIS na magaidi wengine nchini Syria kwa ombi la serikali iliyochaguliwa na wananchi ya Damascus.