Onyo la China kwa Canada kuhusu safari ya wabunge wake Taiwan
China imeionya vikali Canada na kusisitiza kuwa itachukua hatua madhubuti na za nguvu iwapo wabunge wa Canada watafanya safari ya kuitembelea Taiwan karibuni hivi.
Taarifa ya Ubalozi wa China nchini Canada imesisitiza kuwa, safari tarajiwa ya Wabunge wa Canada katika eneo la Taiwan kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari wiki iliyopita, itakuwa na matokeo mabaya katika uhusiano wa Beijing na Ottawa.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Taiwan ni sehemu ya ardhi ya China na Beijing hatuiruhusu nchi yoyote iingilie masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Asia. Kundi la Wabunge wa Canada eti marafiki za Taiwan linatazamiwa kukitembelea kisiwa hicho mwezi Oktoba mwaka huu.
Huku hayo yakijiri, Zheng Zeguang, Balozi wa China nchini Uingereza amewaonya vikali wanasiasa wa nchi hiyo ya Ulaya dhidi ya kuitembelea Taiwan na kusisitiza kuwa, kufuata nyayo za Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi ni sawa na kucheza na moto.

China hivi karibuni ilifanya mazoezi makubwa ya kijeshi kuwahi kushuhudiwa kando kando ya Taiwan, likiwa ni jibu kwa ziara iliyofanywa na Pelosi katika kisiwa hicho. Aidha ilimuwekea vikwazo Pelosi na jamaa zake wa karibu kufuatia ziara hiyo tatanishi.
Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China, na imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan; na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.