Sep 10, 2022 11:33 UTC
  • Mbunge wa Ujerumani: Serikali ya nchi hii ndio 'pumbavu zaidi' barani Ulaya

Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto nchini Ujerumani ameikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kwa kusababisha alichokiita vita 'vibaya' vya kiuchumi dhidi ya Russia.

Sahra Wagenknecht amesisitiza kwa kusema, serikali ya Ujerumani ndiyo "pumbavu zaidi" barani Ulaya kwa kujiingiza katika "vita kamili vya kiuchumi" dhidi ya Russia ambayo ni msambazaji wake mkuu wa nishati.
Akihutubia bunge la nchi hiyo Bundestag, Wagenknecht, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa zamani wa chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke amehimiza kukomeshwa vikwazo dhidi ya Russia na akataka pia makamu wa Kansela na waziri wa uchumi wa nchi hiyo, Robert Habeck ajiuzulu.
Mbunge huyo wa mrengo wa kushoto katika bunge la Ujerumani ameuita mzozo unaoendelea nchini Ukraine "jinai" na kueleza kwamba, vikwazo dhidi ya Russia ni "janga" kwa Ujerumani yenyewe.

Aidha, ametahadharisha kwa kusema: kutokana na kukosekana udhibiti wa bei ya nishati, uchumi wa nchi hiyo karibuni hivi "utabaki kama kumbukumbu tu ya siku nzuri za zamani," na akatoa mwito wa kuondolewa vizuizi na kuanzisha mazungumzo na Russia.

"Kwa kweli tuna serikali ya kijinga zaidi barani Ulaya," amesema Wagenknecht huku akimtaka Makamu Kansela wa nchi hiyo ajiuzulu.
Mbunge huyo amehoji: "ni ujinga gani huu kudhani kwamba tunamuadhibu Putin kwa kuzifukarisha mamilioni ya familia nchini Ujerumani na kuangamiza sekta yetu ya nishati huku Gazprom ikijipatia faida ya juu kabisa?" 
Ulaya inakabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa nishati ambao haujawahi kushuhudiwa kutokana na kuendelea vita vya Ukraine na vikwazo vya Marekani na Magharibi dhidi ya Russia hususan katika sekta ya mafuta na gesi ya nchi hiyo.
Wataalamu wengi wametabiri kuwa nchi za Ulaya zitakabiliwa na hali ngumu sana wakati wa msimu wa baridi kali sambamba na kuongezeka matumizi ya nishati katika nchi hizo.../

Tags