Nov 04, 2022 02:22 UTC
  • China, Russia zapinga mkutano usio rasmi wa Baraza la Usalama la UN dhidi ya Iran

China na Russia zimelaani kuitishwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Wawakilishi wa China na Russia wamelaani kitendo cha Marekani na Albania cha kufanya mkutano usio rasmi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu eti matukio ya Iran.

Mkutano huo uliofanyika kwa anwani ya "Mkutano wa Mfumo wa Arria (Arria-Formula Meetings) kuhusu maandamano ya sasa nchini Iran" ambao umeitishwa na Marekani na Albania, ni sehemu ya juhudi za nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani za kuendeleza machafuko nchini Iran. Katika mkutano huo, mwakilishi wa Russia ameeleza kusikitishwa na kifo cha "Mahsa Amini", lakini pia amebainisha misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi kwa kuashiria mauaji ya "Ashli Babbitt". Babbitt ni mwanamke aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi ya Marekani akijaribu kuingia katika jengo la Congress tarehe 6 January, 2021.  

Ashli Babbitt, alipigwa risasi na kuuawa na polisi ya Marekani akijaribu kuingia kwenye jengo la Congress

Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa pia ameeleza kuwa madhumuni ya mikutano ya Arria Formula ni kutoa ripoti isiyo rasmi kwa wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu masuala yanayohusiana na amani na usalama, lakini masuala ya hivi karibuni ya Iran yalikuwa ndani ya wigo wa masuala ya ndani ya nchi na hayapaswi kuwa katika ajenda ya mkutano wa Arria Formula. 

Mikutano ya Mfumo wa Arria (Arria-Formula Meetings) ni mikutano isiyo rasmi ya Baraza la Usalama ambayo hufanyika kwa kuitishwa na nchi mwanachama. Watu na jumuiya mbalimbali zisizo za serikali wanaruhusiwa kushiriki na kuhudhuria mikutano hiyo kutokana na muundo wake usio rasmi. Mikutano hiyo huwa haifanyika katika jumba la mikutano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wala si jukumu la mkuu wa baraza hilo kutayarisha au kusimamia vikao vyake. Washiriki katika mikutano hiyo pia huhudhuria vikao vyake kwa mujibu wa maamuzi yao binafsi. Kufanyika kwa mikutano hiyo pia huwa hakutangazwi katika jarida rasmi la Umoja wa Mataifa. Inatupasa kuashiria hapa kwamba, mkutano wa Jumatano wiki hii wa Arria-Formula kuhusu matukio ya Iran ulifanyika kwa ushiriki wa ngazi za chini. Kwani ni Marekani na Albania pekee ndizo zilizoshiriki kwa kiwango cha balozi katika mkutano huo. Uingereza na Ireland ziliwakilishwa na manaibu wawakilishi, na wanachama wengine wa Baraza la Usalama kwa ngazi ya wataalamu. Brazil, Mexico, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi tatu za Afrika wanachama wa Baraza la Usalama (Kenya, Ghana na Gabon) zilikuwa na msimamo wa wastani na hazikuzungumza dhidi ya Iran. Mwakilishi wa India hakutoa hotuba katika mkutano huo, suala ambalo linaonyesha mtazamo mzuri wa India kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hotuba yake, balozi wa Venezuela amelaani misimamo ya undumakuwili ya nchi za Magharibi katika uga wa haki za binadamu na hatua za mabavu na za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja zenye malengo ya kisiasa (yaani vikwazo) dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, masuala ya haki za binadamu hayawiani na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran.

Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa linaojumuisha nchi 19, liliamua kusoma taarifa ya kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano huo. Kwa msingi huo, "Joaquín Pérez Ayestarán", naibu mwakilishi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa alienda kushiriki katika mkutano huo, lakini Marekani haikumruhusu kuzungumza kwa kutumia udikteta wake wa vyombo vya habari. Kwa maneno mengine ni kwamba, Marekani haikuruhusu mtu au nchi nyingine yeyote kutoa hotuba isipokuwa yenyewe, wageni na marafiki zake tu. Katika mazungumzo yake na Shirika la Habari la Iran (IRNA), naibu mwakilishi wa Venezuela katika UN amekosoa mienendo hiyo na kinafiki na kindumakuwili ya serikali ya Washington na kusema: Hatua ya Marekani ya kuitisha Mkutano wa Arria Formula dhidi ya Iran katika Umoja wa Mataifa uliojadili hali ya ndani ya Iran ni ukiukaji wa hati ya Umoja wa Mataifa.

Joaquín Pérez Ayestarán

Tangu mwanzoni mwa machafuko nchini Iran, Marekani imejaribu kuendeleza anga ya ghasia na ukosefu wa usalama nchini humo kwa kuweka vikwazo vipya, kufanya propaganda za vyombo vya habari, kuchukua misimamo mikali na kuwahamasisha watu wanaofanya ghasia na machafuko hayo. Ushahidi na nyaraka mbalimbali vinaonyesha kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ushirikiano na mashirika ya kijasusi ya washirika na vibaraka wake, walipanga kuzusha machafuko na pia kutayarisha uwanja wa kuzidishwa mashinikizo ya kigeni dhidi ya Iran.

Taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa, CIA imekuwa na ushirikiano wa karibu na Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Uingereza (MI6), shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD), Idara ya Ujasusi wa Kigeni wa Saudia na nchi nyingine kadhaa katika kutekeleza mpango huo. Hata hivyo harakati hizo zimegonga mwamba; na kutokana na kurejea amani na utulivu nchini Iran, sasa Marekani imeamua kuitisha mkutano usio rasmi wa Baraza la Usalama ikidhani kuwa itaweza kuchochea moto wa ghasia na fujo nchini Iran.  

Tags