Jan 07, 2023 10:21 UTC
  • Shirika la FAO latahadharisha kuhusu taathira za kupanda kwa bei za vyakula

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa limetahadharisha kuwa, kuendelea kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali za vyakula kunatishia usalama wa chakula duniani hasa katika nchi maskini.

Russia na Ukraine ni nchi mbili zilizo na mchango na nafasi muhimu katika kudhamini bidhaa mbalimbali za chakula za kimkakati kama ngano, mahindi na mafuta ya kupikia. Ununuzi wa bidhaa za chakula kutoka Ukraine umepungua sana kufuatia vita vilivyoibuka kati ya  Russia na Ukraine mwishoni mwa Februari mwaka jana; suala ambalo limesababisha matatizo makubwa ya chakula duniani.  

Kupungua uuzaji wa nafaka kutoka Russia na Ukraine kutokana na vita

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, bei ya vyakula duniani mwaka jana iliongezeka kwa asilimia 14.3 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake kutokana na kupanda kwa bei ya nishati na mbolea kulikosababishwa na mapigano kati ya Russia na Ukraine.  

Fahirisi ndogo za shirika la FAO aidha zinaonyesha kuwa, bei ya nafaka mwaka jana ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake yaani 2021 iliongezeka kwa asilimia 17.9, bei ya mafuta ya kula kwa asilimia 13.9, bei za bidhaa zitokanazo na maziwa zikiongezeka kwa asilimia 19.6, nyama asilimia 10.4 na sukari asilimia 4.7.  

Wakati huo huo Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Ulaya hivi karibuni imetangaza kuwa mwezi Desemba mwaka uliopita wa 2022, mfumuko wa bei wa kila mwaka katika nchi 19 za eneo la euro uliongezeka kwa asilimia 9.2.

Tags