Jan 30, 2023 02:48 UTC
  • Mauzo ya silaha za Marekani nje ya nchi yaliongezeka katika mwaka 2022

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa nyaraka zinazoonyesha kuwa, baada ya kuanza vita nchini Ukraine, mauzo ya silaha za nchi hiyo nje ya nchi yaliongezeka sana katika mwaka wa fedha wa 2022.

Kuongezeka mahitaji ya silaha barani Ulaya baada ya vita kati ya Russia na Ukraine, na vile vile katika eneo la Bahari ya Hindi na Pasifiki, sambamba na mashindano ya uundaji silaha yaliyoibuka baina ya Marekani na China, vimepelekea kuongezeka usafirishaji na uuzaji silaha za Marekani nje ya nchi pamoja na kustawi soko la viwanda vya utengezaji silaha vya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zinaonyesha kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2022, ndani ya kipindi cha miezi 12 kilichoishia Septemba 30, 2022, mauzo jumla ya silaha na zana za kijeshi za Marekani kwa nchi za nje yalikuwa ni dola bilioni 51 na milioni 900, ambayo yakilinganishwa na dola bilioni 34 na milioni 800 ya mwaka wa kabla yake ni sawa na ongezeko la 49.1%.

Mnamo mwaka wa 2018, serikali ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump ilizindua mpango mpya uliopewa jina la "Ununuzi wa Zana za Kijeshi za Marekani" ambao ulipunguza vizuizi na kurahisisha zaidi uuzaji wa zana za kijeshi pamoja na kuwashajiisha viongozi wa Marekani wawe na nafasi kubwa zaidi katika kuongeza miamala na biashara za nje katika sekta ya silaha.../