Russia: Wakati wa kustaafu NATO umefika
Akizungumzia kufeli kwa shughuli za Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema wakati wa kustaafu muungano wa NATO umewadia.
Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, amesema baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (NATO) huko Brussels kwamba muungano huo hauna chochote cha kujivunia baada ya miaka 74 ya kuwepo kwake, na kwa hiyo wakati umefika kwamba NATO kustaafu.
Maria Zakharova amesema kuwa hatua na kauli za NATO zinaonyesha kuwa suala la usalama haliendani na shughuli za jumuiya hiyo, na matokeo haya yanaonyesha kuwa ni wakati wa muungano huu wa kijeshi kuhitimisha kazi zake.
Matamshi ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia yametolewa baada ya Finland kujiunga na NATO. Finland ilijiunga rasmi na NATO Jumanne, Aprili 4 licha ya maonyo makali ya Russia.
Maafisa wa Russia wameonya kuwa kujiunga kwa Finland katika jumuiya ya NATO kutazidisha hatari ya kuibuka mapigano.
Ikizungumzia tukio hilo Jumanne iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitangaza kwamba Helsinki imepoteza utambulisho na uhuru wake kwa uamuzi huu.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilisisitiza kwamba kujiunga kwa Finland na NATO kunaweza kuwa na athari mbaya kwa uhusiano wa pande mbili hizo.