Jun 17, 2023 11:06 UTC
  • Biden: Kesi za ufyatuaji risasi zinaripotiwa kila siku nchini Marekani

Rais Joe Binden wa Marekani ameungama na kusema kwamba, matukio ya ufyatuaji risasi na mauaji ya halaiki kwa silaha za moto yameongezeka kwa kiasi cha kutisha nchini humo.

Biden amesema kesi za ufyatuaji risasi zinaripotiwa kila siku nchini Marekani na kwamba, juhudi za kupiga marufuku bunduki au kudhibiti silaha hizo zimeendelea kukabiliwa na upinzani kutoka kwa wazalishaji wa bunduki na waungaji mkono wa 'haki ya kikatiba' ya raia kubeba silaha.

Biden amesema, "Tutaishinda sekta ya bunduki, si rahisi lakini tutawashinda wanasiasa ambao wamekataa kusimama na kuchukua hatua ya kudhibiti umiliki wa silaha za moto nchini." Ikiwa na watu zaidi ya milioni 330, Marekani ina bunduki milioni 400 zilizo mikononi mwa raia.

Takwimu rasmi za hivi karibuni zilizotolewa kuhusiana na ufyatuaji risasi na mauaji ya umati hasa katika shule za Marekani zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka 5 ya hivi karibuni, kumeripotiwa matukio zaidi ya 5,000 katika shule mbalimbali nchini Marekani na kusababisha mauaji na watu kujeruhiwa.

Sehemu moja ya ripoti hiyo inabainisha kwamba, kuanzia mwaka 2018 hadi sasa zaidi ya matukio 1050 ya ufyatuaji risasi moja kwa moja yameripotiwa kutokea katika shule mbalimbali nchini Marekani.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wanauawa kwa silaha za moto kote Marekani kila mwaka, ambapo kwa wastani nchi hiyo inanakili vifo 116 kwa siku. Matukio 647 ya ufyatuaji risasi kiholela yalirekodiwa mwaka wa 2022 ambapo watu 44,287 waliuawa.

Tags