China yakosoa mauzo mapya ya silaha za Marekani kwa Taiwan
China imekosoa vikali mpango mpya wa serikali ya Marekani wa kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya mamilioni ya dola, ikisisitiza kuwa mauzo hayo yanakiuka kanuni ya "China Moja".
Tan Kefei, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesema leo Jumatano katika taarifa kuwa, "China inapinga vikali mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan, na tayari imekabidhi malalamiko yake rasmi kwa Washington."
Kauli ya Tan Kefei imetolewa baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kusema kuwa imeidhinisha mkataba wa kuiuzia silaha Taiwan utaogharimu dola milioni 440.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa China ameeleza bayana kuwa, Marekani imepuuza malalamiko na wasiwasi wa Beijing, na mauzo hayo ya silaha yanaashiria uingiliaji wa mambo ya ndani ya China kwa shabaha ya kuchochea taharuki katika Lango Bahari la Taiwan.

Hivi karibuni pia, Wang Wenbin, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China aliionya Washington kuhusu kuendelea kuiuzia Taiwan silaha akisisitiza kuwa, baadhi ya maafisa nchini Marekani wanataka kuitumia Taiwan kuidhibiti China, lakini wanapaswa kujua kwamba vitendo hivi ni hatari sana, na ni sawa na kucheza na moto.
Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na kwamba chaguo la kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho lipo mezani.