Nov 27, 2023 05:26 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 4

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya mnayoitegea sikio kutoka mjini Tehran. Katika vipindi vitatu vilivyopita tulizungumzia kwa kifupi historia ya ardhi ya Palestina. Katika kipindi chya leo tutazungumzia sehemu nyingine muhimu ya historia hiyo, karibuni.

Wakati Mtume Muhammad bin Abdallah (saw) alipoteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Nabii na Mtume wake kwa ajili ya kuwaongoza walimwengu wote kupitia dini tukufu ya Uislamu, Palestina ilikuwa chini ya utawala wa serikali ya Byzantine, na kwa sababu hiyo, sehemu kubwa ya ardhi hiyo ililazimika kufuata dini iliyoletewa na wavamizi. Ardhi ya Palestina inakumbusha kumbukumbu zenye thamani kubwa kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu na familia yake. Ardhi hii ndiyo ilikuwa njia kuu ya safari za majira ya kiangazi ya wafanyabiashara kutoka Makka kwenda Sham (Syria) ambapo Mtume (saw) kabla ya kupewa Utume alitumia rasilimali alizopewa na Bibi Khadijah (Ummu al-Mu'minin) kufanya biashara na akipitia njia hiyo akiwa na misafara ya wafanyabiashara. Palestina pia kwa Mtume (saw) ilihuisha kumbukumbu ya babu yake Hashim bin Abd Manaf, ambaye amezikwa katika miji wa Gaza. Abdullah bin Abdul Muttalib, baba yake Mtume Muhammad (saw) pia alifariki akiwa katika moja ya safari zake za kibiashara nchini Syria.

Lakini kinachofanya ardhi ya Palestina kuwa na umuhimu maradufu kwa Mtume Mtukufu na wafuasi wake ni kuwepo kwa mji wa Quds (Bait al-Maqdis) na maeneo mengine matakatifu kama vile Msikiti wa Al-Aqsa na Qubatu Swakhra (Kuba la Mwamba) katika ardhi hiyo.

Beit al-Muqaddas ni mji ulio karibu na kitovu au katikati mwa ardhi ya Palestina, takriban kilomita 24 magharibi mwa Bahari ya Chumvi na kilomita 56 mashariki mwa Bahari ya Mediterania, kati ya Uwanda (ardhi tambarare) wa Mediterania na Bonde la Mto Jordan. Mji huo unachukuliwa kuwa mji wenye milima ambao uko futi 2,500 (kama mita 760 hivi) juu ya urefu wa Bahari ya Mediterania na futi 3,800 (kama mita 1,160 hivi) juu ya urefu wa Bahari ya Chumvi. Hali ya hewa ya mji huo ni ya kitropiki, nusu kame, na yenye msimu wa joto kali na kavu na msimu wa baridi huandamana na baridi kali na mvua.

Mji wa Betul Muqaddas ni moja ya miji mikongwe zaidi duniani na moja ya maeneo matakatifu zaidi ambapo Mitume wa Mwenyezi Mungu walizaliwa na kukulia. Mji huo ulitekwa, kuharibiwa na kujengwa upya mara nyingi. Kila sehemu ya ardhi hiyo ina hadithi ndefu ya watu na makabila tofauti yaliyoishi huko na hivyo kuchukuliwa kuwa sehemu takatifu na tukufu duniani. Ni mashuhuri kwamba ni Mitume wa Mwenyezi Mungu ndio walioasisi na kuujenga mji huo. Sehemu hiyo ni makao ya Mitume tokea Nabii Ibrahim hadi Isa (as) (Yesu Kristo) na eneo la kuteremkia Wahyi (ufunuo) na vitabu vitakatifu vya mbinguni kama vile Torati, Injili, Zaburi na vitabu vinginevyo vya mbinguni kabla ya kuteremshwa Qur'ani Tukufu.

Kama tulivyoashiria katika kipindi kilichopita, Nabii Dawood na Suleiman (as) walitawala katika mji huo na wakajaliwa utukufu na adhama. Pia, umuhimu mwingine wa kihistoria wa mji huo, ni kubashiriwa Nabii Zakaria (as) habari njema ya kuzaliwa Nabii Yahya (as) katika mji huo. Mwenyezi Mungu aliamrisha milima na ndege katika mji wa Beitul Muqaddas kutii amri ya Nabii Dawood (as). Isa Masih (as) Yesu Kristo alipaa mbinguni kutokea mjini hapo na imepokelewa kwamba Bibi Maryam aliaga dunia akiwa katika mji huo. Mji huo pia ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu na kwa mujibu wa imani ya Uislamu, ardhi hiyo itakuwa uwanja wa vita vya mwisho kati ya wema na uovu na ni katika ardhi hii ndipo Dajjal atauawa na Mahdi Muahidiwa (af).

Masjidul Aqsa

Masjidul Aqsa ambayo inapatikana katika mji wa Beitul Muqaddas (Jerusalem) ni moja ya maeneo matakatifu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu na kwa Waislamu. Msikiti huo kama tulivyotangulia kusema ni Kibla cha kwanza cha Waislamu ambapo katika zama za utume wa Mtume Muhammad Mustafa (as) ambapo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, alikuwa akiswali na Waislamu akielekea msikiti huo. Vile vile msikiti huo ni wa tatu kwa utukufu baada ya Misikiti ya Masjidul Haram mjini Makka na Masjidu Nabii mjini Madina. Kwa mujibu wa wanahistoria, Masjidul al-Aqsa ni msikiti wa pili kujegwa katika uso wa ardhi baada ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu, Masjidul Haram (Kaaba) mjini Makka, ambao ulijengwa kimsingi kwa ajili ya kuabudiwa Mwenyezi Mungu. Riwaya zinasema kuwa msikiti huo ulijengwa na Nabii Adam (as) miaka 40 baada ya kujengwa al-Kaaba (Beitullah al-Haram), kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Riwaya nyingine, Nabii Ibrahim (as) alijenga upya Kaaba naye Nabii Musa (as) akaamrishwa na Mwenyezi Mungu kuifanya Beitul Muqaddas kuwa Kibla kwa lengo la kuepusha Msikiti wa al-Aqsa kufanyiwa ibada za shirk na upotovu.

Kwa mujibu wa tuliyosema, Beitul Muqadd uliendelea kuwa mji mtakatifu na kuheshimiwa na dini zote hadi wakati alipoteuliwa Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa (saw) kuwa Mtume ili apate kuwafikishia walimwengu ujumbe wake, na hiyo ilikuwa miaka 609 baada ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as). Baada ya kudhihiri jua la Uislamu, Mtume Muhammad (saw) aliruhusiwa na Mwenyezi Mungu kuufanya Msikiti wa al-Aqsa kuwa Kibla cha Waislamu, bila shaka kwa muda tu, na hii ni kwa sababu katika kipindi hicho cha mwanzo wa Uislamu Kaaba ilikuwa imejaa miungu na masanamu ya mushrikina. Kaaba ilikuwa imegeuzwa kuwa jumba la masanamu na kama Waislamu wangeswali na kufanya ibada zao wakiwa wameelekeza nyuso zao huko, bila shaka hiyo ingekuwa aina fulani ya kutukuzwa masanamu hayo, jambo ambalo halikubaliki kabisa katika Uislamu.

Kwa msingi huo, kutokana na kuwa katika kipindi hicho Uislamu ulikuwa ungali mchanga na usio na nguvu ya kutosha, Mwenyezi Mungu alimtaka Mtume wake aelekeze uso wake upande wa Beitul Muqaddas anaposwali, kwa sababu Beitul Muqaddas kilikuwa kibla cha Mayahudi ambao walikuwa wafuasi wa mojawapo ya dini za Tauhidi zinazompwekesha Mwenyezi Mungu. Dini yao ilikuwa karibu zaidi na Uislamu, ikilinganishwa na dini za mushirikina waliokuwa wakiabudu masanamu mjini Makka. Katika kipindi chote alichokuwa akiishi Makka na hata miezi 17 baada ya kuhajiri kwenda Madina, yaani tangu robo ya kwanza ya mwaka wa kwanza hadi nusu ya mwezi Rahab mwaka wa pili Hijiria, Mtume na wafuasi wake walikuwa wakiswali swala zao wakiwa wameelekea Msikiti wa al-Aqsa.

Baada ya hapo Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Mtume na wafuasi wake wabadili kibla na kuswali wakiwa wameelekea Kaaba. Umuhimu wa ardhi ya Palestina na Beitul Muqaddas na hasa Msikiti wa al-Aqsa kwa Uislamu na Waislamu hauishii katika tukio hilo pekee bali unarejea katika tukio jingine lillilotokea tarehe 27 Rajab al-Murajjab, mwaka wa 10 Hihiria (631) ambalo si jingine bali ni tukio la Mi'raaj, yaani kupaishwa mbinguni Mtume Mtukufu (saw), tukio ambalo linatajwa kuwa mojawapo ya miujiza yake mikubwa ya kielimu na kimatendo.

Picha ya miraaj ya Mtume ambayo ilichorwa na Mahmoud Farshchiyan kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

Miraaj ni safari ya kupaa mbinguni Mtume Mtukufu (saw) ambayo ilifanyika kuanzia Masjidul Aqsa. Kwa mujibu wa Riwaya za Kiislamu, Mtume Mtukufu alikuwa Makka alipoteremkiwa na Malaika Jibril ambaye alimwomba aandamane naye kuelekea njia ambako pia kulikuwa na Malaika wengine Mikail na Israfil. Walipokuwa huko, Jibril alimwandalia Mtume farasi kwa jina Buraq ambaye walimpanda na kisha kuelekea Masjidul Aqsa kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Wakiwa huko aliwaswalisha Mitume wengine ili kwa njia hiyo kudhihirisha mamlaka ya Uislamu juu ya dini nyinginezo na kutokea hapo akapaa kwenda mbinguni. Inasemekana kuwa alipaa mbinguni kutokea eneo la Qubatu Swakhra (Kuba la Mwamba). Eneo hilo limepewa jina hilo kwa sababu ya kuwepo kwenye jengo hilo mwamba ambao Mtume (saw) alisimama juu yake muda mfupi kabla ya kupaa mbinguni. Mazungumzo yaliyofanyika kati ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) yamezungumziwa kwa urefu katika Hadithi Qudsi ambayo inaitwa kwa jina hilo yaani 'Hadith Mi'raaj.'  Ni katika kipindi hicho ndipo swala tano tunazoswali kila siku leo ziliwajibishiwa Waislamu. Kisha Mtume (saw) alirejea Quds Tukufu na baada ya hapo akarejea Makka. Ni tangu wakati huo na kuendelea ndipo Palestina na Quds Tukufu zikawa na umuhimu mkubwa na maalumu kwa Waislamu.