Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (130)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kukutana nanyi tena katika kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambapo leo tuko katika sehemu ya 130 ya mfulululo wa vipindi hivi vya itikadi ya Kiislamu.
Swali la kipindi cha leo linasema, je, aya inayozungumzia kukamilika dini na neema ya Mwenyezi Mungu inatuelekeza kwenye Uimamu wa Imam Ali peke yake au na Maimamu wengine watoharifu wa kizazi cha Mtume Mtukufu (saw)? Tunarejea kwenye maandiko matakatifu ili tupate jibu la swali hili muhimu, karibuni.
********
Kwanza tunaashiria sababu ya kuteremshwa aya hii kwenye Hija ya mwisho ya Mtukufu Mtume (saw) ambapo wanazuoni na maulama wengi waliofanya uhakiki wa Qur’ani kuhusian ana aya ya 76 ya Surat al Maida inayosema: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake; na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.
Kwa hakika uzingatia wa aya hii unamuongoza kila mtu mwenye insafu na uadilifu hata kabla ya kurejea kwenye riwaya na hadithi tukufu zinazozungumzia sababu ya kuteremshwa kwake, kufahamu kwamba kuna jambo muhimu mno ambalo lilimteremkia Mtume Mtuku (saw) kutoka kwa Mwenyezi Mungu akimtaka awabainishie watu. Bila shaka aya hii inaonyesha wazi kwamba jambo hilo ni muhimu sana katika ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) kiasi kwamba kama hangelibainisha na kuwafafanulia watu ni kana kwamba hangekuwa amefikisha asili ya ujumbe huo. Kwa msingi huo jambo hilo linaoonekana kuwa nguzo muhimu ya dini ya Mwenyezi Mungu na kudumu kwake. Ni wazi kutokana na madhumuni ya aya hii kwamba Mtume (saw) alikuwa akiogopa kutangaza jambo hilo aliloamrishwa na Mwenyezi Mungu kulifikisha kwa watu kwa kuhofia radiamali na jinsi watu wangesema baada ya yeye kulibainisha. Ni kutokana na hofu hiyo ndipo Mwenyezi Mungu akaahidi kumlinda na watu na kutoruhusu radiamali yao kuzuia utangazwaji wa amri Yake. Chanzo cha radiamali hiyo bila shaka walikuwa ni makafiri ambao hawakuamini kikweli ujumbe wa Mtume Muhammad (saw), hata kama walijidhihirisha kuwa ni Waislamu. Na kwa hivyo Mwenyezi Mungu amehitimisha aya hiyo kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.
Hivyo basi je, ni amri gani hii ambayo Mwenyezi Mungu alimuamrisha Mtume wake kuitangaza? Hapa tunazirejea riwaya za wanahistoria ili tupate jibu sahihi la swali hili.
**********
Kuna maelezo mengi ambayo yamefafanuliwa na wanahistoria wengi wa madhehebu ya pande zote mbili za Shia na Suni kuhusiana na suala hilo, ambapo al-Allama al-Amini amesema katika kitabu chake cha al-Ghadir na vilevile wanazuoni wa Kisuni katika utafiti wao wa kielimu kwamba aya hii iliteremka katika tukio la al-Ghadir ambapo Mtume Mtukufu (saw) alimtangaza Amir al-Mu’mineen Ali (as) kuwa khalifa na walii wa Waislamu baada yake yeye Mtume. Lakini jambo hilo halikuhusiana na Imam Ali (as) pake yake kama tutakavyoona katika maandiko matakatifu, bali liliwajumuisha Maimamu wengine wote kumi na wawili kutoka kizazi cha Mtume Mtukufu (saw). Mwanzoni Mtume (saw) alihofia kutangaza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, kama tulivyosema, kwa kuhofia radiamali na maneno ya watu. Chanzo cha hofu hiyo kilitokana na taasubi na misimmamo ya kikabila na kijahili ya zama hizo, ambayo haingestahamili kuona Utume na Uimamu ukiwekwa kwenye ukoo mmoja kati ya koo za Kureish ambao ni ukoo wa Bani Hashim. Hili ni jambo ambalo linabainishwa wazi na maneno ya Makureishi wenyewe wakiwemo masahaba mashuhuri. Vitabu muhimu vya historia vinasema wazi kwamba koo na makabila ya Qureih hayangelistahamili kuona ukhalifu ukibanwa kwenye ukoo mmoja tu hata kama hilo lingekuwa linatokana na amri ya Mwenyezi Mungu mwenyewe. Makureishi walikuwa wamezoea kugawana uongozi na nyadhifa katika koo zao zote, kama ilivyokuwa kwa mfano, kuhusu suala la kutoa huduma kwenye al-Kaaba, kuwapa Mahujai maji na kuwasaidia na mambo mengine kama linavyothibiti hilo kwenye vitabu vya historia. Kwa hivyo Makureishi walikuwa wakitazamia hilo kutekelezwa kuhusiana na suala la ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) hata kama Mwenyezi Mungu mwenyewe amesema bayana kwamba Yeye ndiye anayefahamu sehemu ya kuweka ujumbe wake. Mila na tabia za kale za Makureishi zilikuwa zingali zinawatawala na kuwadhibiti kiasi kwamba Mtume Mtukufu (saw) alihofia asije akaibua hisia hizo za kijahili kwa kutangaza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu ya kizazi chake kitakatifu kipewa jukumu la kuwaongoza Waislamu kwa amri yake Mola wa ulimwengu. Kutokana na kuwa Mtume (saw) ni mwenye huruma kubwa kwa watu, hivyo alihofia adhabu ya Mwenyezi Mungu isije ikawapata kutokana na upinzani wao dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu ya kumwamuru Mtume atangaze kizazi chake kichukue nafasi ya uongozi wa Umma wa Kiislamu baada ya kuondoka yeye. Na kweli jambo hilo lilitokea ambapo Mwenyezi Mungu alimuepusha Mtume wake na fitina ya makafiri hao wa Kikureishi mara tu baada ya kumtangaza Imam Ali (as) kuwa khalifa na kiongozi wa Waislamu baada yake, kama anavyoashiria Mwenyezi Mungu jambo hilo katika aya za mwanzo za Surat al-Maarij. Tutafafanua suala hilo hivi punde.
********
Imenukuliwa katika Tafsir Majmau al-Bayaan hadithi ambayo al-Hakim al-Hasakani as-Shafi’ anamnukuu Imam Swadiq (as) akiwanukuu babu zake kwamba: ‘Mtume (saw) alipomteua Ali (as) alisema: Na yule ambaye mimi ni Maula wake (msimamizi wa mambo yake) basi huyu Ali ni Maula wake, Habari hizo zilienea kote nchini ambapo an-Nu’man bin Harith al-Fahri alimkujia Mtume (saw) na kumwambia: Umetuamrisha kuhusu Mwenyezi Mungu kwamba tushuhudie kuwa hakuna mungu isipokuwa Allah na kwamba wewe ni Mtume wake, na ukatuamrisha jihadi, hija, swaumu, swala na zaka na tukakubali. Kisha haukuridhika na hayo yote hadi ukamteua kijana huyu kwa kusema: Yule ambaye mimi ni Maula wake basi na Ali ni maula wake. Je, jambo hili ni lako mwenyewe au ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu?
Mtume (saw) akasema: Naapa kwa Allah ambaye hakuna mungu mwingine isipokuwa Yeye, hakika jambo hili linatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hapo Nu’man bin Harithi akaondoka huku akiwa anasema: Wallahi kama huu ni ukweli basi tuteremshie mvua ya mawe kutoka mbinguni. Hapo Mwenyezi Mungu akamdondoshea jiwe kichwani na kumuua. Hapo ndipo Mwenyezi Mungu aliteremsha aya inayosema: Mwenye kutaka alitaka adhabu itakayotokea.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji inabainika wazi kwamba aya inayosema: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, inabainisha wazi umuhimu wa suala la Uimamu na Wilaya ambapo dini ya kweli inasimama juu ya msingi wa suala hili. Wanahistoria wa madhehebu zote mbilia za Shia na Suni wanasema kwamba utangazaji wa kile Mtume (saw) aliteremshiwa na Mwenyezi Mungu ulijumuisha kuteuliwa Imam Ali (as) kuwa khalifa wa Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw). Hilo lilitimia katika hotuba aliyoitoa katika siku ya Ghadir ambapo pia alitangaza Uimamu wa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw) kupitia Hadithi ya Thaqalain, yaani vitu viwili vizito kwa thamani, ambayo aliizungumzia kwenye hotuba hiyo.
Kwa msingi huo aya hii itakuwa inazungumzia Uimamu wa Maimamu wote kumi na wawili wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (saw) na sio Imam Ali (as) peke yake. Hili ndilo suala tutakalolijadili na kuashiria hadithi kadhaa kuhusiana nalo katika kipindi chetu kijacho Inshallah. Basi hadi wakati huo, tunahitimisha kipindi chetu hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kama kawaida mmekitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu Iran ikiwatangazia kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.