Mar 21, 2024 03:07 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 21 Machi, mwaka 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Ramadhani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Machi mwaka 2024.

Katika siku kama yya leo miaka 2197 iliyopita lilianzishwa bunge la kwanza la Iran kwa jina la "Mahestan".

Wabunge wa bunge hili, ambalo liliundwa wakati wa utawala wa mfalme wa Kiashkani, Mehrdad I, walikuwa wanamfalme na wakuu wa Iran. 

Miongoni mwa mamlaka ya Bunge la Mahestan ilikuwa kumhagua na kumuuzulu mfalme iwapo atapatwa na ugonjwa mbaya, wazimu, kutokuwa na uwezo na kusaliti nchi, na vilevile kutangaza vita na kupendekeza suluhu. 

Siku kama ya leo miaka 1448 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bibi Khadija binti Khuwailid mke mwema na kipenzi wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Makka.

Bibi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka, aliolewa na Mtume Muhammad (saw) miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bibi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Uislamu. Kuweko Bibi Khadija (as) pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume (saw) alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa.

Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bibi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib, kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib, ami yake Mtume (saw), pia alifariki dunia mwaka huo huo.

Siku kama ya leo miaka 256 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.   

Joseph Baron Fourier

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi".

Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi.

Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa katika sura mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi za Magharibi.   

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano makubwa kati ya harakati ya PLO ya Palestina na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan.

Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina. 

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.   

Makamanda wa jeshi la Iran

Na tarehe 21 Machi 1990, nchi ya Namibia ilipata uhuru na kujitenga na Afrika Kusini.

Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia.

Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma. 

Bendera ya Namibia