Sep 20, 2016 06:11 UTC
  • Jumanne 20 Septemba 2016

Leo ni Jumanne 18 Dhulhija 1437 Hijria sawa na tarehe 20 Septemba 2016.

Siku kama hii ya leo miaka 1427 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

Siku kama ya leo miaka 765 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.

Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30, huku likienda kwa mwendo mdogo na liligunduliwa na raia wa Uingereza kwa jina la Gordon Branz. Hii leo mabasi bora na ya kisasa yamegeuka kuwa moja ya vyombo muhimu vya usafiri.

Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mnamo mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa, huku akiwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 sanjari na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za taifa hilo la katikati mwa Afrika.

Tarehe 18 Dhulhija miaka 223 iliyopita alizaliwa faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.