Jumanne, Oktoba 25, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 23 Muharram 1438 hijria sawa na Oktoba 25, 2016.
Siku kama ya leo, miaka 205 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Hadi umri wa miaka 12, Galois hakuwahi kufundishwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alijiunga na chuo akiwa na umri huo na kuanza kusoma vitabu mbalimbali vya taaluma ya hisabati. Aliandika kitabu chake cha kwanza mashuhuri cha hisabati akiwa na umri wa miaka 18 na baada ya hapo aliandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois alifungwa jela kutokana na itikadi zake za kisiasa na aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832.
Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania. Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo. Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica. Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973.
Siku kama ya leo tarehe nne Aban miaka 52 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya kuwapa kinga raia wa Marekani waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba, uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.
Na siku kama ya leo miaka 141 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na "Anisul Muwahhidin".
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita mji wa Khorramshahr wa Iran ulikaliwa kwa mabavu na jeshi la dikteta wa zamani Iraq Saddam Hussein. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Mji huo ulikombolewa tarehe 3 Khordad ambayo inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi.